Habari za Kitaifa

Washukiwa wa mauaji ya Were wakana kuwa wanachama wa genge hatari

Na  JOSEPH WANGUI August 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Watu watatu wanaokKaabiliwa na mashtaka ya kumuua aliyekuwa Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, wamehusishwa na genge hatari la uhalifu linalojulikana kama “Kabreeze” katika kaunti ya Homa Bay.

Hata hivyo, watuhumiwa hao wamekana madai hayo, wakisema kuwa “Kabreeze” ni chama halali cha ustawi wa kijamii kilichosajiliwa.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, genge hilo linajulikana kwa kutumia vurugu na vitisho, na kaka mdogo wa marehemu mbunge, Bw Paul Were, ameripoti kupokea vitisho kutoka kwa ndugu wa mmoja wa washukiwa.

Aidha, imebainika kuwa baadhi ya mashahidi muhimu wa upande wa mashtaka — wakiwemo marafiki na jamaa wa watuhumiwa — wamewekwa chini ya ulinzi maalum wa Serikali baada ya kueleza hofu ya usalama wao.

Kwa misingi hii, Mahakama ya Kibera jijini Nairobi imekataa kuwapa dhamana washukiwa, ikisema kwamba uzito wa mashtaka hayo pamoja na hali ya hatari inayowakabili mashahidi wanaolindwa haufai kupuuzwa.

Washukiwa hao ni William Imoli Shighali almaarufu Imo, Edwin Oduor Odhiambo almaarufu Machuani na Ebel Ochieng almaarufu Dave Calo.

Wote walikuwa wameomba kuachiliwa kwa dhamana wakisubiri kesi yao kusikilizwa. Mawakili wao walidai kuwa dhamana ni haki ya kikatiba, na kwamba wateja wao si watu wa kutoroka, kwani walishirikiana na polisi wakati wa kukamatwa kwao.