Habari za Kitaifa

Washukiwa wa wizi wa watoto Eldoret wazuiliwa

April 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TITUS OMINDE

POLISI mjini Eldoret wamefichua mtandao wa washukiwa wa ulanguzi wa watoto ambapo wafanyakazi wa hospitali ya kibinafsi wanakula njama na walanguzi hao kwa kughushi stakabadhi za kuzaliwa zinazotumiwa na walanguzi kupata vyeti vya kuzaliwa ambavyo hatimaye hutumika kuwasafirisha watoto walioibwa.

Makachero walifanikiwa kunasa wanawake watatu wa umri wa makamo miongoni mwao wakiwa wafanyakazi wawili wa hospitali ya kibinafsi.

Watatu hao walifikishwa mahakamani kuhusiana na makosa yanayohusiana na ulanguzi wa watoto.

Brenda Cheptoo, Rael Nyaboke na Clanca Njeri walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Eldoret Barnabas Kiptoo na kushtakiwa kwa ulanguzi wa watoto wanne wenye umri wa kati ya miezi 7 na miaka 5.

Wakiwa mbele ya mahakama, hawakuruhusiwa kujibu mashtaka baada ya upande wa mashtaka kuomba muda zaidi kukamilisha uchunguzi kuhusu sakata ya ulanguzi wa watoto inayohusishwa na wanawake hao.

Walikamatwa katika mji wa Eldoret siku nne zilizopita na maafisa wa polisi wa DCI na kuzuiliwa katika seli ya kituo cha polisi cha Naiberi katika kaunti ndogo ya Ainabkoi, Kaunti ya Uasin Gishu.

Kulingana na hati za mashtaka, mshtakiwa wa kwanza na wa pili ni wafanyakazi wa hospitali ya Fountain huku mshtakiwa wa tatu akiwa mshiriki wa sakata ya ulanguzi wa watoto.

Walipofikishwa mahakamani, upande wa mashtaka uliwasilisha ombi la kuwazuilia kwa siku 21 wakisubiri uchunguzi ukamilike.

Kupitia hati yake ya kiapo kortini, afisa wa uchunguzi inspekta Joyce Thunge kutoka idara ya DCI Eldoret Mashariki aliambia mahakama kuwa huenda watatu hao wakaingilia uchunguzi iwapo wataachiliwa kabla ya kukamilika kwa uchunguzi.

Aidha, mpelelezi huyo aliiambia mahakama kuwa washukiwa hao walikuwa na uwezekano wa kutokana na uzito wa mashtaka dhidi yao.

Bi Thunge aliambia mahakama kuwa mshukiwa mkuu Bi Cheptoo ndiye anayesimamia rekodi ya hospitali huku Nyaboke akifanya kazi katika kituo hicho kama mtaalamu wa lishe.

Aidha, alifichua kuwa maafisa wa upelelezi wanakusudia kuwafanyia watoto hao wanne vipimo vya DNA ili kuwabaini wazazi wao wa kibayolojia.

Mahakama pia iliambiwa kuwa upande wa mashtaka ulikuwa bado haujarekodi taarifa kutoka kwa mashahidi wakuu katika kesi ya ulanguzi wa watoto.

Mahakama iliagiza polisi kuwazuilia washukiwa hao kwa siku 12 katika kituo cha polisi cha Naiberi hadi uchunguzi ukimilike.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 15.