Washukiwa wanne washtakiwa kwa kutoa shahada ghushi hotelini
WASHUKIWA wanne, akiwemo raia wa Amerika na raia wa Pakistani, wameshtakiwa kwa makosa ya kuwapatia Wakenya watano shahada ghushi zikiwemo za uzamivu baada ya mafunzo ya siku tatu pekee katika Hoteli ya White sands.
Miongoni mwa shahada ghushi zilizotolewa ni Shahada tatu za Uzamili katika Usimamizi wa Biashara (Uongozi na Usimamizi) na Shahada mbili za Uzamivu (PhD) katika Uongozi.
Washukiwa hao, waliotambuliwa kama Dayis Lawrence Bennett (raia wa Amerika), Farah Akbar (raia wa Pakistani), Ekra Wambui Ndung’u, na Josephine Ndune, walikamatwa na maafisa wa polisi wa kituo cha Bamburi waliovamia hoteli hiyo baada ya kupokea taarifa ya kijasusi.
Wanne hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Shanzu Alhamisi na kushtakiwa kwa makosa matano ya uhalifu, ikiwemo kutoa shahada kinyume na Kifungu cha 28(2) na (3), kama kinavyosomwa pamoja na Kifungu cha 28(5) cha Sheria ya Vyuo Vikuu.
Kwa mujibu wa karatasi ya mashtaka, washukiwa hao, pamoja na wengine ambao hawakufikishwa mahakamani, walijiwasilisha kama mawakala wa taasisi ya kigeni na kwa njia isiyo halali wakatoa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uongozi kwa Purity Kimotho Wakuhu na Issack Alio Hassan bila idhini kutoka kwa Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE).
Katika mashtaka mengine, walidaiwa kutoa kwa njia isiyo halali Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara katika Uongozi kwa Evely Mila, Sepiso E.L. Nalumango, na Ahmed Noor Hassan bila idhini inayohitajika.
Mahakama iliambiwa kuwa, makosa hayo yalifanyika Februari 12, katika Hoteli ya Whitesands, Bamburi.
Hata hivyo, washukiwa walikana mashtaka yote walipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Shanzu, Leah Juma.Bennett na Akbar waliomba kupewa dhamana wakidai walikuwa na matatizo ya kiafya yanayohitaji uangalizi wa mara kwa mara.
Kupitia kwa wakili wao, walihakikishia mahakama kuwa hawana nia ya kutoroka na kuwa wako tayari kufuata masharti yote ya mahakama.Kesi hiyo itatajwa tena Februari 18.