Habari za Kitaifa

Washukiwa wawili wakamatwa kwa kumchinja mbwa

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA FRIDAH OKACHI

POLISI kutoka kituo cha Mutuini wanawazuilia wanaume wawili waliopatikana na nyama ya mbwa katika mtaa wa Kirigu, Dagoretti Kusini, jijini Nairobi.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, washukiwa hao walipatikana wakimchinja mbwa na kupakia nyama kwenye gunia.

Bw Sammy Kamau, ambaye ni mmojawapo wa wakazi wa eneo hilo, alisema alipokea taarifa kutoka kwa mpitanjia kuwa aliwaona watu kwenye kichaka kimoja wakimchinja mbwa.

Bw Kamau, alichukua jukumu la kutafuta majirani wengine waliondamana naye hadi kwenye eneo la tukio.

“Juzi tulipata gunia la nyama za mbwa na Jumanne washukiwa hao walipatikana wakimchinja mbwa na kisha wakipakia nyama kwenye gunia. Mimi nilipodokezewa suala hilo, nilitafuta wenzangu ambao tulishirikiana na kweli tukawafumania,” alisema Bw Kamau.

“Kutoka hapa hadi kichinjio cha ng’ombe na mbuzi si mbali. Lakini vijana wamengeuza vichaka vilivyo karibu kuwa vichinjio vya wanyama mbalimbali na kusambaza nyama kuuziwa wateja ambao hawana ufahamu,” aliongeza.

Baada ya kuwafumania, wakazi hao walimpigia simu naibu chifu wa eneo hilo, Bw Samson Rono, ambaye aliwafahamisha polisi.

Akithibitisha kisa hicho Bw Rono alisema nyama iliyopatikana ni ya mbwa wawili waliokuwa wamechinjwa. Bw Rono alisema kuwa wanaume hao walitekeleza kitendo hicho Jumanne mwendo wa saa kumi na moja asubuhi.

“Baadhi ya nyama zilikuwa zimepakiwa kwenye gunia tayari zikisubiri kuchukuliwa. Wawili hao wanazuiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea,” alisema Bw Rono.

Bw Rono aliwataka wakazi ambao hawana ajira kutojihusisha kwenye biashara haramu ya kuwachinja wanyama kinyume cha sheria.

“Hata ikiwa huna kazi, ni hatia kujitafutia riziki kwa kuwaua wanyama ovyoovyo. Unawaua wanyama bila kujua ni hatari gani unaletea jamii,” aliongeza Bw Rono.