Habari za Kitaifa

Wasioamini Mungu wataka wapewe holidei baada ya Ruto kuahidi kutenga ya Wahindi, Diwali

Na CHARLES WASONGA October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SAA chache baada ya Rais William Ruto kutangaza kuwa serikali itadhamini mswada wa kutenga Novemba 1, kila mwaka kuwa sikukuu ya kitaifa kusherehekea Diwali, wasiomwamini Mungu pia wanataka watengewe sikukuu mahsusi.

Diwali ni tamasha la Kihindu linaloadhimishwa kwa ufyatuliaji wa fataki na hufanyika kati ya Oktoba na Novemba. Inahusishwa na miungu ya ufanisi kwa jina, Lakshmi.

Kwenye taarifa, Rais wa kundi la watu hao nchini (Atheist in Kenya Society-AKS) Harrison Mumia Jumatano alisema watawasilisha ombi katika Bunge la Kitaifa Ijumaa wiki hii (Novemba 1, 2024) wakitaka kuanzishwa kwa Siku ya Kitaifa ya Wasioamini Mungu.

“Sikukuu hiyo itakuwa ni kuwatambua watu ambao wameasi imani ya kidini (haswa imani kwa Mungu wa Israel, Yahweh, Mungu wa Waarabu, Allah na miungu ya Wahindu) na badala yake wamekumbatia ubinadamu, usasa na fikra huru,” anasema Mumia.

Anasema hatua ya AKS inalandana na hitaji la Kipengele cha 27 cha Katiba kwamba serikali haitabagua mtu yeyote kwa misingi yoyote ile “ikiwemo dini, mawazo na imani”.

Mumia na wenzake watawasilisha ombi hilo bungeni siku ambayo jamii ya Wahindu watakuwa wakishiriki tamasha za Diwali.

Rais Ruto aliahidi kuwa serikali itageuza Diwali kuwa sikukuu ya kitaifa alipokutana na wawakilishi wa jamii ya Kihindu nchini katika Ikulu ya Nairobi, Jumatano.

Kiongozi wa taifa aliahidi kuzungumza na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ili ahakikshe kuwa mswada wenye pendekezo hilo unapitishwa na wabunge kabla ya hafla ijayo ya Diwali Novemba mwaka wa 2025.

“Nimesikia ombi lenu kwamba Diwali ichukuliwe kama sikukuu ya kitaifa. Litashughulikiwa na bunge na Spika yuko hapa,” Dkt Ruto akasema.

“Nitaongea naye ahakikishe kuwa mswada wa kufanikisha ombi hili umepitishwa. Kwa hivyo, ningetaka kuwahakikishia kuwa tutakuwa tumeamua kufikia Diwali ijayo,” akaeleza.

Naye Bw Mumia alitishia kuwa endapo Bunge litakataa ombi lao watawasilisha kesi kortini.

Hata hivyo, hakupendekeza tarehe wala mwezi ambao wangetaka Sikukuu ya Wasiomwamini Mungu iadhimishwe.