Habari za Kitaifa

Wasiwasi kuhusu maandalizi Sekondari Pevu ikianza Januari 12

Na LYNET IGWADAH December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MASWALI yameibuka kuhusu uwezo wa shule kuhudumia wanafunzi wapya wanaotarajiwa kujiunga na Sekondari Pevu mwakani.

Haya yanajiri huku Waziri wa Elimu, Julius Ogamba akisema shule zina uwezo wa ziada na Wizara ya Elimu inatarajia asilimia 100 ya wanafunzi 1.13 milioni kujiunga na Sekondari Pevu.

Hata hivyo, baadhi ya wakuu wa shule wanahisi hawako tayari kikamilifu. Wakuu wa shule waliozungumza na Taifa Leo wameelezea wasiwasi wao kuhusu mkondo wa Sayansi, Tekinolojia na Hisbati (STEM) kutokana na ukosefu wa miundombinu ya ICT na vifaa.

“Tunasema wanafunzi 1.13 milioni watajiunga na shule za sekondari huku uwezo wa shule ukiwa 1.5 milioni, tuko sawa na tunatarajia asilimia 100 ya wanafunzi ambao matokeo yao tumeyatoa leo,” alisema Katibu wa Elimu ya Msingi, Julius Bitok, jana wakati wa uzinduzi wa matokeo ya KJSEA.

Bw Ogamba alisema nafasi katika shule 9,540 za sekondari zitaongezeka wanafunzi 929,262 watakapomaliza shule za sekondari baada ya Mtihani wa (KCSE) mwaka huu.

Wanafunzi watateuliwa katika shule za sekondari kulingana na Makundi- 1 hadi 4 -kulingana na utendaji wao na mkondo waliyochagua—STEM, Sanaa na Michezo, na Sayansi za Jamii.

Hata hivyo, ukibaki mwezi mmoja tu kabla ya tarehe ya kuripoti ya Januari 12, 2026, vitabu vya Kiingereza pekee ndivyo vilivyofikishwa shule.

Hii imesababishwa na deni la Sh10 bilioni wanazodai wachapishaji. Aidha, baadhi ya shule hazina maabara za kompyuta zinazofanya kazi na zinashindwa kulipa madeni ya vifaa vilivyonunuliwa.

“Mbali na kutokuwa na kompyuta, tuna madeni ya vifaa vya maabara ikiwemo kemikali,” alisema mkuu wa shule ambaye hakutaka kutajwa jina.

Mkuu mwingine wa shule anakadiria kuwa kubadilisha darasa moja kuwa maabara ya kompyuta kutagharimu takriban Sh700,000, pesa ambazo hawana.