Habari za Kitaifa

Wasiwasi magaidi wakilenga kwa mara nyingine kambi za GSU Lamu

Na KALUME KAZUNGU July 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIKOSI vya kulinda usalama msituni Boni, Kaunti ya Lamu, vimezidisha msako dhidi ya magaidi wanaohusishwa na kundi la Al-Shabaab, baada ya jaribio jingine la kuvamia kambi ya polisi wa GSU.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, magaidi hao wamejaribu kuvamia kambi za GSU kwenye vijiji tofauti vya msitu wa Boni lakini majaribio yao yakatibuliwa.

Kisa cha hivi majuzi zaidi ni kile cha Ijumaa usiku, ambapo magaidi wapatao 60 wa Al-Shabaab waliojihami kwa silaha hatari walijaribu kuingia katika kambi ya GSU Basuba kwa lengo la kuilipua lakini wakakabiliwa vikali na kushindwa nguvu.

Uvamizi huo ulitekelezwa majira ya saa tatu unusu usiku, ambapo magaidi walijitokeza msituni na kuanza kufyatua risasi kila upande kuilenga kambi hiyo.

Pia walijaribu kurusha makombora kwa mbali (RPG) ili kuimaliza kambi hiyo lakini wakashindwa nguvu, hivyo kutokomea kwenye vichaka vya msitu wa Boni.

Jaribio lao la kuvamia wakazi wa kijiji cha Basuba pia lilitibuliwa na askari wa akiba (NPR) wanaolinda kijiji hicho.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Wesley Koech, alithibitisha shambulio hilo lakini akasisitiza kuwa hali imedhibitiwa vilivyo.

Alisema maafisa wa vitengo mbalimbali vya usalama wametumwa Basuba na msitu wa Boni ili kuendeleza oparesheni ya kuwasaka wahalifu hao.

Aliwataka wananchi kuondoa shaka na kuwasihi kushirikiana na vitengo vya usalama kumkabili na kumwangamiza adui.

“Oparesheni kali inaendelea msituni Boni. Doria za walinda usalama zimeongezwa. Kufikia sasa hakuna mhalifu aliyekamatwa. Wananchi washirikiane nasi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kumshinda adui,” akasema Bw Koech.

Mbali na uvamizi wa kambi ya GSU na kijiji cha Basuba mnamo Ijumaa, Al-Shabaab pia wamejaribu kuvamia sehemu zingine.

Mnamo Julai 15 mwaka huu, maafisa watatu wa Jeshi la Kenya (KDF) waliuawa huku sita wengine wakijeruhiwa gari lao liliposhambuliwa kwa kilipuzi cha kutegwa ardhini (IED) eneo la Badaa, karibu na Sankuri msitu wa Boni.

Mnamo Julai 13, magaidi walijaribu kuvamia kambi ya GSU kijijini Milimani lakini wakakabiliwa vilivyo na maafisa hao na kushindwa nguvu.

Aprili 5, magaidi hao walivamia kijiji cha Basuba na kambi ya GSU iliyoko karibu lakini wakashindwa nguvu na polisi pamoja na askari wa akiba (NPR) walioko kijijini.

Mnamo Machi 15, magaidi wa Al-Shabaab walivamia kijiji cha Mangai, ambapo waliwakusanya watu mahali pamoja na kuwahubiria mafundisho ya itikadi kali.

Baadaye waliwagawia tende kabla ya kutokomea katika msitu wa Boni.

Visa vinavyojirudiarudia vya Al-Shabaab kuvamia kambi za walinda usalama na wanavijiji msituni Boni vinashuhudiwa wakati ambapo oparesheni ya kuwasaka magaidi hao imekuwa ikiendelea katika eneo hilo tangu Septemba 2015.

Operesheni hiyo kwa jina ‘Amani Boni’ ilizinduliwa na serikali, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza au kuwafurusha magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu mkuu wa Boni.

Hali hii imewafanya wakazi vijijini Boni kuishi kwa hofu, wakitaka kuwe na kambi za kijeshi karibu na sehemu ambazo huvamiwa mara kwa mara.