Habari za Kitaifa

Wasiwasi vitabu vya CBC vikikosekana shule zikikaribia kufunguliwa

Na DANIEL OGETTA December 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUKU shule zikikaribia kufunguliwa, wazazi na walimu wanakumbwa na changamoto kufuatia kucheleweshwa kwa orodha ya vitabu vilivyokubaliwa rasmi kutumika kuanzia darasa la tano hadi la nane.

Wazazi hao wanahofia kucheleweshwa huku na Taasisi ya Ukuzaji Mtaala (KICD),  kunaaathiri kujiandaa kwa watoto wao  kabla ya muhula mpya kuanza, huku nao wakikabiliwa na changamoto za kifedha.

“Hatuelewi. Tunatarajiwa vipi kupanga masomo ya watoto wetu bila orodha ya vitabu?” mzazi mmoja aliuliza.  Wazazi wengi hununua vitabyu wakati wa likizo.

Mtaala wa Elimu na Utendaji (CBC) unategemea vifaa rasmi vya masomo ili kufanikisha malengo yake kwa wanafunzi.

Bila vitabu, walimu wanakosa mwongozo wa kufanikisha ratiba za masomo, hali inayoweza kuathiri mafunzo shuleni.

Wazazi hao wanahofia kuwa KICD inahatarisha elimu ya watoto, hasa wakati nchi inakumbwa na changamoto za katika utekelezaji wa CBC.

Kucheleweshwa huku pia kumeziacha shule nyingi zikiwa hazijaweza kujiandaa ipasavyo, hali inayotishia kuvuruga ratiba za masomo shule zitakapofunguliwa.

Wakuu wa shule wameelezea wasiwasi wao, wakionya kwamba bila kupatikana kwa vitabu vilivyokubaliwa kwa wakati, shughuli za kufundisha na kujifunza zitakumbwa na changamoto kubwa.

“Hili ni kosa kubwa. CBC inategemea mwongozo uliopangiliwa vizuri, na bila vifaa hivi, tunaanza muhula kwa njia ambayo si dhabiti,” alisema mkuu mmoja wa shule.

 Hata hivyo, KICD imekanusha madai ya kuwa imechelewa kutoa vitabu, ikisema vitabu vinapatikana shuleni na katika maduka ya kuuza vitabu.

Mkurugenzi wa KICD Prof Charles Ong’ondo, alisema vitabu vya masomo yote kuanzia masomo ya chekechea hadi darasa la tisa vipo tayari tena madukani.

Lakini alikiri kuwa vitabu vya masomo ya Kilimo, Sanaa za Ubunifu, na Mafunzo ya kiufundi kwa darasa la saba na nane vilikamilishwa Desemba hii.

“Vitabu hivi bado havijachapishwa, lakini vinatarajiwa kwenye maduka ifikapo Februari 2025,” akasema.

Prof Ong’ondo alieleza kuwa kuchelewa huko kulitokana na mchakato wa kuboresha mtaala kufuatia ripoti ya Kamati ya Rais ya Marekebisho ya Elimu iliyotolewa Agosti 2023.

Kwa sasa, kuna upungufu wa vitabu vya lugha ya Kifaransa katika shule zote nchini,  baada ya serikali kupeana mkandarasi biashara ya kuchapisha vitabu milioni moja vya Kifaransa ambavyo havikua vinahitajika shuleni.

Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu, alisema matumizi ya fedha kwa vitabu hivi hayakuzingatia thamani yao.

 Hata hivyo, Prof Ong’ondo alieleza kuwa Kifaransa na lugha nyingine za kigeni si somo la lazima kwa madarasa ya kwanza hadi tisa. Shule zinazofundisha masomo haya zimeombwa kutoa taarifa kwa KICD ili kusaidia kupanga usambazaji wa vitabu.