Wasiwasi wavulana wengi wakizaliwa Kenya kuliko wasichana
KENYA ilirekodi idadi kubwa ya watoto wa kiume waliozaliwa mwaka wa 2024 kuliko wa kike, hali ambayo wataalamu wanatahadharisha kuwa inaweza kuathiri usawa wa kijamii katika siku zijazo.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kiuchumi ya 2025 iliyotolewa Alhamisi, wavulana 570,807 walizaliwa mwaka jana ikilinganishwa na wasichana 539,706 – na hivyo kuwa na wavulana 106 kwa kila wasichana 100.
Hii ni tofauti ya zaidi ya wavulana kwa wasichana kuzaliwa katika kipindi cha zaidi ya mwongo mmoja.
Shirika la Kitaifa la Takwimu ya Kenya (KNBS) linaeleza kuwa wavulana wamekuwa wakizaliwa kwa wingi kuliko wasichana kila mwaka tangu 2015.
Kwa mara ya kwanza, shirika hilo pia limerekodi rasmi kuzaliwa kwa watoto wa jinsia mbili. ambapo watoto tisa walisajiliwa mwaka wa 2024, ikilinganishwa na wanne mwaka uliotangulia.
Ingawa faida ya kuzaliwa kwa wavulana inalingana na mienendo ya kimataifa, baadhi ya wanajamii wanaelezea wasiwasi wao. Utafiti wa Kituo cha Pew Research Centre wa mwaka wa 2022 ulionyesha kuwa ingawa kawaida wavulana huzaliwa kwa idadi kubwa kuliko wasichana, wanawake huishi kwa muda mrefu na wana viwango vya chini vya vifo, hivyo kuwa wengi katika makundi ya umri mkubwa.
“Mwaka 2021, wanawake walikuwa asilimia 56 ya watu duniani wenye umri wa miaka 65 na zaidi. Wanatarajiwa kuwa asilimia 54 ifikapo 2050,” utafiti huo ulisema, ukieleza tofauti za kibaiolojia na kitabia kuwa sababu ya vifo vya juu kwa wanaume.
Hata hivyo, nchini Kenya – ambako baadhi ya jamii bado zinapendelea watoto wa kiume – mwelekeo huu wa muda mrefu wa idadi ya wanaume kuzidi wanawake unaweza kuleta changamoto za kijamii.
Mwanajamii Dkt Roselyter Riang’a anaonya kuwa na wanaume wengi kuliko wanawake kwa muda mrefu kunaweza kuleta upungufu wa uwiano katika ndoa.
“Ikiwa hali hii itaendelea, huenda tukaona wanaume wengi wanaofaa kuoa kuliko wanawake, hali ambayo inaweza kuwaathiri wanaume wasiojiweza kiuchumi,” alisema.
Anaongeza kuwa hali hii inaweza pia kusababisha mienendo isiyo ya kawaida katika familia: “Huenda tukaona vijana wanaume wakianzisha ndoa na wanawake wakubwa – mara nyingi akina mama wasio na waume – wanaotafuta wenza na utambulisho wa kijamii kupitia ndoa.”
Ingawa taifa linaweza kufaidika na nguvu kazi kubwa za wanaume, wataalamu wanaonya kuwa hali inaweza kuwa na athari zisizotarajiwa za kijamii iwapo haitashughulikiwa.