Wataalamu: Kupandisha ushuru hakutaongeza mapato ya serikali
WATAALAMU wa bajeti wameiambia Wizara ya Fedha kuwa kuwaongezea Wakenya mzigo wa ushuru hakutasaidia serikali kufikisha malengo yake ya mapato na bado utawala huu utaendelea kukopa hela.
Haya yanafanyika huku ikibainika kuwa serikali ilikosa kufikia malengo yake ya kifedha kwa Sh342 bilioni ndani ya miaka miwili iliyopita ya kifedha.
Ufichuzi huo ulitokana na ripoti iliyotolewa na Afisi ya Bajeti ya Bunge (PBO).
Kiasi hiki ni cha juu zaidi kuliko kile ambacho hazina ya kitaifa ya fedha ilikuwa imesema Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) ingekusanya kama mapato ya ziada kwa muda ambao sheria mpya za ushuru zimekuwa zikitumika.
Kuokoa jahazi, afisi ya bajeti bungeni imeiambia serikali ifikirie upya kuhusu mbinu yake ya ushuru.
Afisi hiyo ambayo ina jukumu la kushauri bunge kuhusu masuala ya kifedha, imeitaka serikali ikumbatie uwekezaji ili kuziba mianya ya mapato madogo yanayokusanywa.
“Serikali miaka michache iliyopita imepanua mawanda yake ya ukusanyaji ushuru kuongeza mapato yake kwa kutumia sheria mpya za ushuru. Hata hivyo, mapato yanayokusanywa yanaendelea kuwa chini huku umma nao ukiendelea kughadhabishwa na sheria mpya za ushuru,” ikasema stakabadhi ya PBO.
Pia, afisi hiyo imesema mapato ya chini yamechangiwa na utekelezaji duni wa sheria za kifedha na mfumo usioeleweka wa kusimamia ushuru.
Ripoti ya PBO inaonyesha kuwa mapato ya chini yalishuhudiwa 2023/24 na 2024/25 wakati ambapo sheria mpya za ushuru zilianza kutekelezwa.
Kwa mfano mnamo 2023/24, kupitia Sheria ya Fedha 2023, serikali ilikuwa ikilenga kukusanya Sh211 bilioni. Hata hivyo, ilinoa kwa sababu malengo ya kukusanya mapato hayo yalikosa kutimia kwa Sh205 bilioni.
Mwaka wa kifedha 2024/25, Mswada wa Fedha 2024 ulikuwa umesema KRA ilikuwa ikilenga Sh346 bilioni. Hata hivyo, mswada huo haukutekelezwa baada ya Wakenya kuandamana kuupinga, kilele cha maandamano hayo kikiwa vijana kuvamia majengo ya bunge mnamo Juni 25, 2024.
Kuokoa hali, serikali iliibuka na sheria za kifedha ambazo zililenga kukusanya Sh79 bilioni. Hata hivyo, malengo ya mapato ya mwaka huo yalikosa kutimia kwa Sh137 bilioni na serikali ikalemewa na shinikizo za kifedha hadi ikaongeza uwezo wake wa kukopa ndani na nje ya nchi.
Kwenye mwaka wa kifedha wa 2025/26, serikali inalenga kukusanya mapato ya Sh3.3 trilioni na inalenga Sh30 bilioni kupitia ushuru kwenye Sheria ya Fedha 2025.
“Badala ya kuongeza ushuru, serikali inastahili kuhakikisha kuwa mfumo unaotumika unaziba mianya inayotumika kukwepa ushuru,” ikasema ripoti ya PBO.
PBO imeonya kuwa ushuru wa asilimia tano kwa pesa zinazoondolewa na wacheza kamari huenda zikasababisha wajiondoe kwenye majukwaa ya kamari yanayoeleweka.
Kupitia kamari, serikali inalenga kupata kati ya Sh5.4 bilioni na Sh11.4 bilioni. Ushuru unaolengwa utawaingiza wachezaji kamari hofu na watorokee kampuni za kamari ambazo hazidhibitiwi.
Kwa kawaida, ushuru wa asilimia 20 ndio umekuwa ukitozwa kwenye pesa ambazo washindi wa kamari wanazipata.