Watatu wakana kumlaghai mwekezaji Sh129 milioni
WAFANYABIASHARA watatu wanashtakiwa kumlaghai mwekezaji Sh129 milioni.
Wanadaiwa kuahidi kumchukulia Shahzada Aniq Ayub kibali cha kufanya kazi nchini na leseni ya kununua na kuuza vyuma vikuukuu.
Watatu hao Ibrahim Ahamed Ibrahim, Abdul Zarak Rehan na Mohammed Suleiman walishtakiwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Mahakama ya Milimani Martha Nanzushi.
Walikana kumlaghai Ayub, mwekezaji kutoka ng’ambo, kitita cha Dola za Marekani USD ($) 881,009.71 sawa na Sh113,650,256.30 na Sh15,337,500 zote zikiwa jumla ya Sh129,187,756.
Mashtaka yalisema washtakiwa hao walimlaghai Ayub pesa hizo kati ya Desemba 4,2023 na Juni 6,2024 jijini Nairobi.
Rehan alishtakiwa peke yake kwa ughushi wa leseni ya kuuza na kununua vyuma vikuukuu.
Kiongozi wa mashtaka Herbert Sonye hakupinga washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana ila alimsihi hakimu azingatie kiwango cha pesa alichopoteza Ayub.
Kila mmoja aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.
Kesi hiyo itatajwa mnamo Septemba 10,2024 kutengewa siku ya kusikizwa baada yao kushtakiwa Agosti 28.