Watatu wauawa maandamano yakienea Indonesia
Jarkata, Indonesia
Watu watatu wameuawa baada ya waandamanaji kuchoma moto jengo la bunge mashariki mwa Indonesia, huku maandamano ya kitaifa yakiendelea kufuatia kifo cha mwendesha pikipiki.
Affan Kurniawan, mwenye umri wa miaka 21, aligongwa na gari la polisi jijini Jakarta wakati wa maandamano ya awali kuhusu mishahara midogo na matumizi ya kifahari ya wanasiasa, maandamano ambayo bado yanaendelea.
Maandamano haya yanachukuliwa kama jaribio kubwa kwa Rais Prabowo Subianto, ambaye alitembelea familia ya Kurniawan Ijumaa jioni kutoa rambirambi zake.
Jumamosi, rais huyo alifuta ziara aliyopanga kwenda China wiki ijayo kuhudhuria gwaride la kijeshi kuadhimisha mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kufuatia machafuko yanayoendelea kote nchini Indonesia.
Jukwaa la mitandao ya kijamii la TikTok pia limeamua kusitisha huduma ya matangazo ya moja kwa moja nchini humo kwa muda wa siku chache kutokana na maandamano hayo.
Waandamanaji walikusanyika mwishoni mwa wiki, wakiwemo waliokusanyika mbele ya makao makuu ya polisi huko Bali, moja ya maeneo maarufu ya watalii nchini humo. Polisi katika maeneo mbalimbali walitumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Mazishi ya Affan Kurniawan yalifanyika Ijumaa, yakihusisha wenzake waliomsindikiza hadi kwenye makao yake ya mwisho.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na mkuu wa polisi wa Jakarta Asep Edi Suheri, pamoja na wanasiasa Rieke Dyah Pitaloka na gavana wa zamani wa Jakarta, Anies Baswedan, ambao walieleza matumaini kuwa tukio hilo litachunguzwa kwa kina, lakini pia waliwataka waendesha bodaboda kusitisha maandamano yao ili kudumisha utulivu.
Mkuu wa polisi alitoa tena msamaha kuhusu tukio hilo.
Wakati haya yakiendelea, waandamanaji walikusanyika nje ya makao makuu ya polisi wakitaka haki itendeke kwa kifo cha Kurniawan.
Rais Subianto pia ametoa msamaha kwa familia ya Kurniawan, akisema kuwa alishtushwa na kufadhaishwa na hatua za kupita kiasi zilizochukuliwa na maafisa wa polisi.
Gavana wa Jakarta, Pramono Anung, naye alitembelea familia ya marehemu Kurniawan, akitoa pole na msaada wa kifedha kwa mipango ya mazishi.