Habari za Kitaifa

Watu 21 wafariki katika ajali ya basi Kisumu

Na ANGELINE OCHEING August 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Watu 21 wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la shule lililokuwa limewabeba waombolezaji katika eneo la Mamboleo Coptic, Kaunti ya Kisumu.

Mkuu w Trafiki katika eneo la Nyanza  Peter Maina, alithibitisha vifo hivyo Alhamisi, akisema kuwa watu wengine watano walijeruhiwa vibaya huku 15 wakipata majeraha madogo.

Waathiriwa wote walioponea ajali hiyo wanapokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) mjini Kisumu.

Kulingana na taarifa ya awali, basi hilo lilikuwa likirejea kutoka mazishini kabla ya kupinduka kwa sababu ambazo bado hazijabainika.

Maafisa wa uokoaji, wakiwemo maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu na polisi, walifika katika eneo la tukio kwa haraka kusaidia waathiriwa na kuendesha shughuli za uokoaji.