Watu 339 wametuma maombi wakitaka kusimamia IEBC; tutateua saba kwa uwazi – Jopo
MAKAMISHNA wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) watakuwa kazini kufikia Aprili 25, jopo lililoteuliwa kuunda tume hiyo limesema.
Jopo linaloongozwa na Dkt Nelson Makanda lilifichua hayo Jumanne katika Hoteli ya Enashipai mjini Naivasha ambako limekuwa likikutana.
“Kufikia sasa tumepokea maombi kutoka kwa watu 339 kujaza nafasi saba zilizotangazwa, ikiwa ni pamoja na ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi. Sisi, kama jopo la uteuzi, tunajizatiti kuhakikisha kwamba tunatimiza wajibu wetu wa kuwapa Wakenya mwenyekiti ajaye na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kufikia Aprili 25,” Dkt Makanda alisema.
Kulingana na jopo hilo, maombi mengi yaliwasilishwa kupitia mtandao.
“Majina ya waombaji wote na ratiba ya kuhoji watakaoorodheshwa itachapishwa katika magazeti, na Tovuti ya Tume ya Huduma ya Bunge, alieleza Dkt Makanda.
Makamu mwenyekiti wa jopo hilo, Lindah Kilome aliwahakikishia Wakenya kuwa litatekeleza shughuli ya kuwaajiri makamishna kwa njia ya haki, uwazi na bila upendeleo.
Baada ya mchujo na mahojiano, jopo litawasilisha majina ya wahitimu kwa Rais William Ruto kuteuliwa kuhudumu katika IEBC.
Rais Ruto kisha atateua mmoja kuwa mwenyekiti na watu sita kuwa makamishna.