Habari za Kitaifa

Watu 8 wafariki katika ajali nyingine ya barabarani Kitengela

Na  Stanley Ngotho August 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Watu saba wamefariki dunia na wengine wakijeruhiwa vibaya katika ajali mbaya ya barabarani eneo la Korompoi, Kitengela, kwenye barabara kuu ya Nairobi–Namanga.

Ajali hiyo ilitokea saa mbili asubuhi na kuhusisha lori na matatu ya kubeba abiria 14. Matatu hiyo, iliyokuwa imejaa abiria, ilikuwa ikielekea Kitengela huku lori likielekea upande wa Isinya.

Kwa mujibu wa walioshuhudia, lori hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi na lilikuwa likijaribu kupita gari lingine lililokuwa mbele yake kabla ya kugongana na matatu iliyokuwa ikitoka upande wa pili. Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

“Kulikuwa na ukungu mzito sana leo. Madereva walikuwa wakiendesha magari yao wakiwa wamewasha taa. Nilikuwa naendesha nyuma ya matatu kwa umbali mfupi kabla ya kusikia mlipuko mkubwa ukifuatiwa na kilio na kelele. Nilisimama mara moja na kugundua kuwa ilikuwa ajali mbaya sana. Miili kadhaa ilitupwa nje ya matatu huku mingine ikinaswa ndani,” alisema John Njogu, dereva wa tuk-tuk.

Wakazi wa eneo hilo wamelalamikia ukosefu wa matuta katika eneo hilo ambalo limebainika kuwa hatari. Wanasema ajali zimekuwa za kawaida, ambapo watu wasiopungua saba wamepoteza maisha katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, akiwemo mama na mtoto wake waliogongwa na lori lililokuwa likiendeshwa kwa kasi wiki tatu zilizopita.

Wakazi waliokuwa na hasira waliteketeza lori hilo na kuandamana kwa kufunga barabara, wakitaka matuta na alama za barabarani kuwekwa mara moja.

Wakazi pia wametoa wito kwa Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) pamoja na maafisa wa trafiki kufanya msako mkubwa dhidi ya madereva wanaokiuka sheria za barabarani na kuhatarisha maisha ya wengine.

“Tunataka hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti ajali hizi ambazo zimekuwa kawaida. Ajali zimekuwa jambo la kawaida. Mashirika husika yaingilie kati mara moja ili kuokoa maisha,” alisema Ann Ndunge, mkazi wa eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Isinya, Simon Lokitari, alithibitisha vifo hivyo na kutoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu ili kuepuka ajali.

Amesema visa vya madereva kuendesha magari kwa kasi ni vingi kwa sababu wanadhani kuwa barabara hiyo haina msongamano mkubwa wa magari.

“Ni asubuhi ya huzuni sana. Tumepoteza watu saba wanawake wanne na wanaume watatu, wote wamefariki papo hapo. Kuna waliojeruhiwa vibaya na wamekimbizwa katika hospitali mbalimbali kwa matibabu,” alisema Bw Lokitari.

Barabara ya Nairobi–Namanga ina sifa ya kuwa na idadi kubwa ya malori yanayosafirisha bidhaa kutoka nchi jirani ya Tanzania kupitia mpaka wa Namanga.

Pia, hakuna maeneo maalum ya kuvukia mifugo, jambo ambalo huwalazimu wafugaji kuivusha mifugo yao mahali popote barabarani.

Walioumia wanapokea matibabu katika hospitali mbalimbali, huku miili ya waliopoteza maisha ikihifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Shalom na Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela, ikisubiri kutambuliwa na kufanyiwa upasuaji wa maiti.