Habari za Kitaifa

Watu sita wafariki dunia katika ajali ya barabarani

Na  WYCLIFFE NYABERI  July 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Watu sita wamethibitishwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika kituo cha kibiashara cha Kijauri kwenye barabara ya Kisii-Sotik Ijumaa jioni.

Ajali hiyo ilihusisha lori, gari la umma aina ya Nissan na lingine dogo la Toyota Premio.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Trafiki katika Kaunti Ndogo ya Borabu Wycliffe Kundu, lori hilo lililokuwa likitoka njia ya Keroka, lilipoteza mwelekeo na kisha kuyagonga magari hayo mawili yaliyokuwa yameegeshwa kando ya barabara.

Afisa huyo aliongeza kuwa baada ya kugonga magari hayo mawili, lori hilo lilipaa jus ya mtaro mkubwa ulioko eneo hilo kabla ya kutua kwenye vibanda kadhaa vinavyomilikiwa na wafanyabiashara wadogo wadogo.

“Lori hilo lilikuwa limebeba magogo ya miti ambayo yalikuwa yakisafirishwa hadi kiwanda cha chai kilichoko karibu. Dereva wa lori hilo alishindwa kulidhibiti alipokuwa akishuka katika mteremko mmoja ulio eneo hilo. Kisha aligonga magari mawili yaliyokuwa yameegeshwa kando ya barabara na  kuruka mtaro na kutua kwenye vibanda kadhaa sokoni,” Bw Kundu aliambia Taifa Leo kwa simu.

Kamanda huyo aliongeza kuwa kumetokea visa vinginvya ajali katika eneo hilo na hivyo aliwataka madereva kuwa waangalifu wanapoendesha kwenye barabara hiyo.

“Eneo hilo limesababisha ajali nyingi. Tunawaomba watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu zaidi wanapofika huko hasa nyakati kama hizi ambapo mvua inanyesha,” Bw Kundu alisema.

Waliopata majeraha walikimbizwa katika hospitali za karibu kwa matibabu.

Ajali hiyo inajiri mwezi mmoja tu baada ya watu wengine watatu kupoteza maisha katika barabara hiyo hiyo

Watatu hao waliuawa katika mji wa Keroka, kilomita chache kutoka Kijauri.

Zaidi ya watu watano wamefariki dunia jioni hii katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea eneo la Kijauri, barabara ya Kisii–Sotik. PICHA| HISANI

Ajali hiyo ilihusisha matatu aina ya Nissan iliyokuwa ikielekea Keroka kutoka Masimba mjini na pikipiki.

Dereva wa matatu alishindwa kuimudu alipokuwa akishuka kwenye njia ya Ichuni. Wakati akihangaika kulidhibiti gari lake, alimgonga mwendesha pikipiki aliyekuwa mbele yake, na kumuua mwendeshaji huyo na abiria wake . Kisha matatu hiyo ilitua kwenye mtaro na kumeangukia mpita njia mmoja.

Ili kupunguza ajali hizo, Mwenyekiti wa Bodaboda wa Kaunti Ndogo ya Masaba Kaskazini Dominic Babu alitoa wito wa kuhamishwa kwa wafanyabiashara ambao alisema wanauza bidhaa zao karibu na barabara hiyo.

“Wafanyabiashara katika barabara hiyo wamejenga vibanda karibu na barabara kuu na kuna haja ya kuwadhibiti ikiwa tutaepuka ajali kama hizo siku zijazo,” Bw Babu alisema.

Pia aliomba Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu  Kenya (Kenha) kuweka alama mpya barabarani ili kuwaonya madereva na watumiaji wengine.