Habari za Kitaifa

Watu sita wafariki katika ajali ya matatu katika barabara ya Nakuru-Eldoret

Na  TITUS OMINDE October 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 1

Watu sita, akiwemo dereva wa matatu, walifariki dunia baada ya magari matatu kugongana katika eneo la Koriomat, kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Ajali hiyo iliyotokea usiku wa manane ilihusisha lori aina ya Mercedes-Benz Actros, gari aina ya Toyota Succeed na matatu aina  ya Toyota Hiace ya kampuni ya North Rift Sacco iliyokuwa na abiria 10.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Wilberforce Sichirani, alisema lori hilo lilikuwa likitoka Nakuru kuelekea Eldoret lilipokwepa gari jingine lililokuwa mbele yake.

Katika kufanya hivyo, dereva wa lori alikata kona kuelekea upande wa kulia na kugonga Toyota Succeed kabla ya kugonga matatu hiyo.

Nguvu za mgongano huo zilisababisha matatu na Toyota Succeed kutumbukia kwenye mtaro uliokuwa upande wa kulia wa barabara.

Bw Sichirani alisema dereva wa matatu, aliyetambuliwa kama Shabaan Hassan Wanga, na abiria watano wa kike walifariki papo hapo.

Abiria wengine ambao idadi yao haijabainishwa walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika hospitali mbalimbali za Kaunti ya Uasin Gishu kwa matibabu.

Miili ya waliofariki ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, kusubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.

“Tumeanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hii ya kusikitisha,” alisema Bw Sichirani.

Polisi wanaendelea kutambua  waathiriwa wengine na idadi kamili ya waliojeruhiwa.

Mabaki ya magari yaliyohusika katika ajali hiyo yanatarajiwa kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Burnt Forest kwa ukaguzi.

Ajali hiyo inaongeza idadi ya watu wanaopoteza maisha katika ajali za barabarani nchini, huku mamlaka zikiendelea kuonya kuhusu hatari zinazotokana na makosa ya madereva.

Baadhi ya sababu zinazochangia ajali hizo ni pamoja na kupita magari mengine bila tahadhari, mwendo wa kasi na madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa.