Habari za Kitaifa

Watu wawili wafariki katika ajali ya magari kadhaa katika barabara ya Nairobi- Mombasa

Na BENSON MATHEKA August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa vibaya kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea, Jumamosi, Agosti 16, katika eneo la Kwa Mautiiyo, Malili, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Athi River Kusini, David Kandie, ajali hiyo ilitokea saa moja  na nusu asubuhi, baada ya pick up kujaribu kupita trela na kugongana na gari lililokuwa likitoka upande wa pili, kabla ya kusukumwa hadi ikagongana na trela lingine.

Miongoni mwa waliopoteza maisha ni dereva wa trela na kijana wa miaka 25 aliyekuwa ameketi nyuma ya pick up. Majeruhi watatu walikimbizwa katika Hospitali ya Machakos Level 5 na wanapokea matibabu.

Pick up hiyo ilipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kyumbi kwa uchunguzi zaidi huku polisi wakidhibiti haraka eneo la ajali baada ya wakazi kuanza kuchota mafuta yaliyomwagika.

Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa watu 2,933 wamefariki kutokana na ajali za barabarani kati ya Januari na Agosti 10, mwaka huu.