Habari za Kitaifa

Watumishi wa umma kukingwa wasipoteze ajira hata mashirika yakivunjwa

Na DAVID MWERE December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATUMISHI wa umma katika kiwango cha kitaifa na kaunti ambao nyadhifa au mashirika wanamofanyia kazi, yatafutiliwa mbali, watakingwa kutokana na kupoteza ajira, chini ya sheria mpya iliyopendekezwa.

Iwapo Mswada kuhusu Huduma ya Umma na Usimamizi wa Wafanyakazi 2024, ambao umewasilishwa kwa Bunge la Kitaifa, utapitishwa kuwa sheria jinsi ulivyo kwa sasa, waajiriwa ambao nyadhifa zao zitafutiliwa mbali hawatapoteza ajira lakini watajumuishwa kwingineko.

Mswada huo umejiri huku kukiwa na ripoti kuhusu futafuta za serikali kwa lengo la kuangazia idadi kubwa kupita kiasi ya watumishi wa umma. Inakadiriwa kuwa wafanyakazi milioni moja wananyofoa zaidi ya Sh1 trilioni kupitia mishahara.

Umejiri vilevile wakati ambapo wafanyakazi wa Bima ya Afya Nchini (NHIF) wanakabiliwa na sintofahamu huku uhamisho wa Mamlaka ya Afya kwa Jamii (SHA) ukizidi kutekelezwa baada ya sheria kubadilishwa.

Japo serikali imewahakikishia kulinda kazi zao, hakuna hatua thabiti kuwa watadumishwa chini ya SHA, kuhamishwa au kujumuishwa katika asasi nyingine ya umma.

Mawasiliano ya awali kutoka kwa serikali yalisema maafisa walioajiriwa chini ya NHIF watahitajika kutuma upya maombi ya kazi chini SHA, na hakuna hakikisho wataajiriwa tena.

Ina maana kuwa, wale watakosa kufanikiwa baada ya kuhojiwa, watalazimika kukabiliana na hali zao kila mtu kivyake.

Mswada uliowasilishwa na Mbunge wa Runyenjes Eric Muchangi, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Leba katika Bunge la Kitaifa, unalenga sheria saba zitakazobadilishwa kwa lengo la kufanyia mageuzi usimamizi wa waajiriwa katika utumishi wa umma,” Kwa huduma bora ya utumishi wa umma ili kuwezesha utowaji huduma bora.”

“Afisa hataondolewa waka kulazimishwa kustaafu kutoka utumishi wa umma kwa misingi ya afisi kuvunjiliwa mbali isipokuwa pale taasisi ya utumishi wa umma imeona inafaa kumpa mafunzo upya, kumtuma au kumhamisha mtumishi wa umma,” unasema Mswada huo katika kipengee cha 13.

“Mswada huu unanuiwa kuimarisha utumishi wa umma ili Wakenya waweze kuhudumiwa vyema na kuwezesha maendeleo nchini kulingana na malengo ya maendeleo.”

Mswada huo unapendekeza kuwa taasisi ya utumishi wa umma katika viwango vyote viwili vya kitaifa na kaunti, itaunda mwongozo wa kuanzisha na kufutilia mbali afisi kulingana na Sheria kuhusu Tume ya Huduma ya Umma.

“Uamuzi wa taasisi ya umma kuhusu kuvunjilia mbali afisi katika huduma ya umma utazingatia sheria husika na mchakato wa kutuma, kuhamisha, kuondoa, au kustaafisha maafisa walioathirika au katika masharti yanayohusu afisa wa umma,” unaeleza Mswada huo.