Habari za Kitaifa

Watumishi wa umma kulipa pesa taslimu kwa huduma zikidai SHA malipo ya miezi 9

Na ANGELA OKETCH August 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Hospitali za binafsi kote nchini sasa zimeamua kutowahudumia tena watumishi wa umma bila malipo ya pesa taslimu, kufuatia kile zinazotaja kuwa  serikali kushindwa kulipa madeni ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kwa kipindi cha miezi tisa.

Watumishi wote wa umma – wakiwemo wanaofanya kazi katika wizara, mashirika ya serikali, idara, na kaunti – isipokuwa walimu na maafisa wa polisi, watalazimika kulipa pesa taslimu ili kupata huduma katika hospitali zote binafsi iwapo SHA na Wizara ya Afya hazitaingilia kati kuzuia utekelezaji wa agizo hilo jipya.

Katika barua rasmi iliyotumwa Agosti 7, 2025, Shirikisho la Huduma za Afya Kenya (KHF) lilimjulisha Afisa Mkuu Mtendaji wa SHA, Dkt Mercy Mwangangi, kuwa hospitali za kibinafsi hazitaweza tena kubeba mzigo wa kifedha wa kuwahudumia watumishi wa umma bila kulipwa.

“Isipokuwa madeni haya yaliyosalia yalipwe kulingana na makubaliano ya mkataba, watoa huduma hawatakuwa na budi ila kuwaomba watumishi wa umma walipe bili zao zote – za awali na zijazo – kisha wawasilishe maombi ya kurejeshewa fedha na waajiri wao au SHA,” aliandika Dkt Kanyenje Gakombe, Mwenyekiti wa KHF.

Shirikisho hilo limetangaza “kutoweza kuendelea kutoa huduma kwa mkopo kwa watumishi wa umma”, hali ambayo inaweza kubadilisha kabisa uhusiano kati ya hospitali za kibinafsi na mpango wa bima ya afya wa serikali.

KHF, kama vile bodi ya sekta ya afya ya Muungano wa Sekta ya kibinafsi Kenya (KEPSA), inajumuisha hospitali za kibinafsi, mashirika ya kitaaluma, na wahudumu wengine wa afya wa sekta wasio wa serikali. Ilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma bora na nafuu za afya kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi.

Barua hiyo ilinakiliwa kwa viongozi wa mashirika makuu ya afya kama Muungano wa Hospitali za Kikristo (CHAK), Muungano wa Hospitali za Vijijini na Mijini (RUPHA), Muungano wa Hospitali za kibinafsi Kenya (KAPH), vyama vya madaktari wa meno na mashirika ya maduka ya dawa.

KHF sasa inataka malipo ya moja kwa moja kutoka kwa wagonjwa kwa huduma yoyote watakazopata katika hospitali za kibinafsi hadi deni la miezi tisa lilipwe kikamilifu.