Habari za Kitaifa

Waumini 10,000 wa kundi la Dawoodi Bohra wala chakula cha kiroho Mombasa

May 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WACHIRA MWANGI

ZAIDI ya waumini 10,000 wa kundi la Dawoodi Bohra wamekusanyika Mombasa kwa mahubiri na kupokea baraka kutoka kwa kiongozi wao wa kiroho, Dkt Syedna Mufaddal Saifuddin.

Kiongozi wao ambaye cheo chake ni Al-Dai al-Mutlaq wa 53, aliwasili Mombasa mnamo Ijumaa mchana kutoa mahubiri na kuzungumza na waumini wa jamii hiyo.

Ziara ya Dkt Saifuddin katika kanda ya Afrika Mashariki inafuatia ziara yake ya hivi majuzi Cairo, Misri ambapo alijiunga na Rais wa Misri Abdel Fattah El Sisi kwa uzinduzi wa msikiti na kaburi la Sayyida Zainab.

Alipowasili nchini Kenya, Dkt Saifuddin alifanya ziara fupi katika Aljamea-tus-Saifiyah Nairobi, taasisi kuu ya elimu ya jamii hiyo, ambapo alishiriki katika maandamano ya sherehe na kuongoza swala ya Ijumaa.

Kiongozi wa kiroho wa kundi la Dawoodi Bohra Dkt Syedna Mufaddal Saifuddin akiwa kwa gari alipowasili Mombasa. PICHA | WACHIRA MWANGI

Kilele cha ziara yake kitakuwa ni hotuba ya kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Syedna Abdeali Saifuddin, kiongozi wa 42 wa jamii hiyo, ambaye alikuwa na jukumu muhimu katika kuwaongoza waumini wa kundi la Dawoodi Bohra kutoka Gujarat, India, kwenda Afrika Mashariki zaidi ya karne mbili zilizopita.

Syedna Abdeali Saifuddin pia alianzisha shule ya awali ya Aljamea-tus-Saifiyah huko Surat, Gujarat.

Kuendeleza urithi wake, Syedna Mohammed Burhanuddin, kiongozi wa 52, na Syedna Mufaddal Saifuddin wa sasa, walizindua Shule ya Nairobi ya chuo hicho mwezi Aprili 2017.

Wakati wa kukaa kwake Mombasa, Dkt Saifuddin atazungumza na wanachama wa jamii hiyo, akitoa mwongozo na ushauri kuhusu masuala mbalimbali.

Kiongozi wa kiroho wa kundi la Dawoodi Bohra Dkt Syedna Mufaddal Saifuddin (wa pili kushoto), alipowasili jijini Mombasa mnamo Mei 17, 2024. Waumini 10,000 wa Dawoodi Bohra wanapokea chakula cha kiroho kwa wiki moja wakipata fursa ya kutangamana na kiongozi wao. PICHA | WACHIRA MWANGI

Wanafunzi wote na walimu wa Aljamea walisafiri kwenda Mombasa kushiriki katika hafla na kuadhimisha tukio hilo.

Mratibu wa Jumuiya ya Bohra jijini Mombasa, Bw Hamza Shura, alielezea heshima kubwa ya jamii hiyo kwa kumkaribisha Dkt Saifuddin.

“Kuwasili kwake kunaleta furaha maradufu mwaka huu 2024 kufuatia uzinduzi wa kaburi la Sayyida Zainab, ambalo ni eneo takatifu kwa jamii yetu,” alisema Bw Shura.

Naye Bw Quresh Zakir alisisitiza umuhimu wa ziara hizo, akibainisha kuwa zinatoa nafasi za kiroho na kielimu na fursa za kushiriki katika shughuli za kijamii na uhifadhi wa mazingira.

Mwaka 2023, Dkt Saifuddin alizindua mpango wa kuvuna maji ya mvua kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, lengo likiwa kupunguza uhaba wa maji katika eneo hilo.

Mpango huo ulifanikiwa sana na ulihamasisha miradi kama hiyo duniani kote.