Wazazi sasa kulipa karo kupitia e-Citizen kuzima ukora
NA WANDERI KAMAU
ITAKUWA lazima kwa wazazi na walezi kuwalipia watoto karo kupitia mtandao wa e-Citizen.
Hili ni baada ya Wizara ya Elimu mnamo Ijumaa kutoa agizo, ikiwataka wazazi au walezi wenye wanafunzi katika shule za kitaifa kutumia mfumo huo kuwalipia karo.
Agizo hilo linalingana na mkakati wa serikali kulainisha ulipaji wa huduma zake zote kupitia nambari ya biashara 222222.
Kwenye notisi iliyotumiwa walimu wote wakuu wa shule za kitaifa Januari 3, 2024, Katibu wa Elimu ya Msingi Belio Kipsang, aliwaagiza kuwasilisha nambari ya akaunti ya benki ya shule zao kwa taasisi husika za kifedha ili kufanikisha utekelezaji wa agizo hilo.
“Usimamizi mkuu wa e-Citizen, kwa ushirikiano na Mamlaka ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICTA), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijitali na Wizara ya Fedha zinashirikiana kuweka huduma zote za serikali katika mfumo wa e-Citizen ili kuboresha utoaji huduma,” ikaeleza notisi hiyo.
Ili kuhakikisha uzingatiaji wa mfumo huo, wazazi wanaagizwa kulipa karo kupitia e-Citizen.
Walimu wakuu wameagizwa kutoa maelezo muhimu ya kifedha kwa Afisi ya Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Elimu ya Msingi, kufikia Februari 6, 2024.
Serikali ilisema itatoa mwongozo kuhusu ulipaji wa karo kupitia mfumo huo mpya, baada ya kupokea maelezo yote muhimu yanayohusu akaunti za benki zinazotumia kulipia karo.
Mnamo Juni 2023, Rais William Ruto aliagiza kuwianishwa kwa ulipaji wa huduma za serikali ili kupunguza visa vya ubadhirifu wa baadhi ya fedha.