• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Wazazi wataka madereva wa shule wachunguzwe umri, afya kufuatia ajali za kutisha

Wazazi wataka madereva wa shule wachunguzwe umri, afya kufuatia ajali za kutisha

NA WINNIE ATIENO

WAZAZI wameitaka serikali ya kitaifa kuchunguza madereva wa magari ya shule zote za umma ikiwemo msingi, sekondari na vyuo vikuu ili kuhakikisha wamehitimu kwa mujibu wa sheria za trafiki nchini.

Wakiongea na Taifa Leo, wazazi hao walisema kuongezeka kwa visa vya ajali barabarani kunaendelea kuzua taharuki nchini.

“Tunataka kujua kama hawa madereva wanaoendesha magari ya taasisi za elimu nchini yanayosafirisha watoto wetu wamehitimu,” alisema mwenyekiti wa muungano wa wazazi nchini Bw Silas Obuhatsa.

Bw Obuhatsa alisema wazazi wanaendelea kuwa na wasiwasi huku madereva hao wakisafirisha wanafunzi, kwenye michuano mbali mbali na makwao shule zikifunga kwa muhula wa pili wiki hii.

Walimtaka Waziri wa Elimu Bw Ezekiel Machogu na mwenzake wa Uchukuzi Bw Kipchumba Murkomen kushirikiana kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanaotumia magari ya umma.

“Serikali iliyopita ilikuwa imeweka mikakati kabambe ya usalama barabarani ikiwemo kupiga marufuku magari ya taasisi za elimu kusafiri usiku ili kupunguza ajali barabarani,” aliongeza mwenyekiti huyo.

Bw Obuhatsa, alisema ipo haja ya Bw Machogu na Bw Murkomen kubuni jopokazi maalum la kuchunguza ajali barabarani hasa zinazohusisha magari ya taasisi za elimu za umma.

Alisema kuanzia Januari, ajali nyingi zimetokea na kusababisha maafa ya wanafunzi wengi.

Mnamo Machi 18, wanafunzi 11 wa chuo kikuu cha Kenyatta waliangamia kwenye ajali huko Maungu, Voi, Kaunti ya Taita Taveta katika barabara kuu ya Mombasa kuelekea Nairobi huku wengine 46 wakijeruhiwa.

Wanafunzi hao walikuwa wakielekea Mombasa kwa matembezi ya shule kabla ya basi lao kugongana na lori.

Aprili 1, mwanafunzi wa shule ya upili ya Chavakali aliaga dunia huku wengine 32 wakijeruhiwa baada ya basi walimokuwa wakisafiria kupinduka katika barabara kuu ya Kakamega kuelekea Kisumu.

Februari 24, wanafunzi watatu wa shule ya msingi ya Maadili Junior walifariki na wengine kunusurika na majeraha baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuhusika kwenye ajali katika barabara ya Gitugi kuelekea Murang’a.

Muungano huo ulitoa mapendekezo kadhaa ili kupunguza ajali barabarani.

“Kwanza madereva wote wapigwe msasa kubaini kama wamefuzu kwa mujibu wa sheria za trafiki nchini. Wafanyiwe ukaguzi wa afya na hata umri kutathminiwa. Pengine wanaoendesha watoto wetu hawajahitimu,” alisema.

Bw Obuhatsa alisema magari yanayosafirisha wanafunzi yawekwe vidhibiti mwendo.

“Wazazi wana uchungu wa kupoteza watoto wao kiholelaholela. Shule zinapofungwa tunataka walimu wakuu wawe makini na watoto wetu. Tuepuke ajali, tuokoe maisha,” alisema Bw Obuhatsa.

Alisema maafisa wa trafiki wasiovalia sare za polisi wawekwe sehemu kadhaa ili kushika doria.

Vile vile, Bw Obuhatsa alisema magari ya umma yanayosafirisha wanafunzi yanafaa kuwa na muuguzi ili kusaidia wakati wa majanga.

  • Tags

You can share this post!

Alan Shearer: Mtarajie mabadiliko juu ya jedwali la EPL...

Jombi achekwa na marafiki kwa kukiri babake alimsaidia...

T L