Waziri Machogu afichua kijana wa mwavuli alikuwa na nia nzuri
NA MWANGI MUIRURI
WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu ameshangaa kusikia uvumi kwamba kuna mvulana ambaye alijaribu kumvamia alipofika akamfunika kwa mwavuli mjini Murang’a mnamo Januari 15, 2024.
Kisa hicho kilitokea katika uwanja wa Mumbi ulioko viungani mwa mji wa Murang’a wakati wa hafla ya kutoa basari kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Kijana huyo alijitokeza ghafla akiwa amebeba mwavuli na akamkinga waziri kutokana na jua kali lililokuwa likichoma utosi wa kila mmojawapo aliyefika uwanjani alasiri hiyo.
Wasaidizi wa Bw Machogu walionekana kuingiwa na wasiwasi na ndipo mmoja alikimbia kuchukua jukumu hilo la kumkinga dhidi ya miale ya jua.
Aidha, Bw Machogu alisikika akiwaelekeza wasaidizi wake waachane na huyo kijana kwa sababu “ni rafiki yangu”.
Waziri pia alimwelekeza msaidizi wake aliyekuwa amechukua jukumu la kumkinga jua na mwavuli aache.
Sasa, Bw Machogu amesema kwamba “huyo mvulana hakuwa na nia mbaya ila tu alitaka kuwa karibu nami ndiposa aone namna ambavyo ninamsaidia”.
Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa ufadhili wa masomo wa Benki ya Kenya Commercial mnamo Januari 17, 2024, waziri alionekana kuchanganyikiwa na uvumi kwamba maisha yake yaliwekwa hatarini na mtoto wa shule.
“Huyo kijana alikuwa anataka kuwa karibu nami akingojea usaidizi wa sare ya shule, karo, na viatu na niliwajibika,” akasema Bw Machogu.
Alisema ni kawaida viongozi kutafutwa ili watatue changamoto mbalimbali.
Alisema yeye na Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang pamoja na maafisa wa usalama wanaowalinda, huwa hawazingatii sana kuzima visa kama hivyo vya walio na haja ya kusaidiwa.