Weita amuua mpenziwe mwanafunzi wa KMTC siku nne kabla ahitimu
MWANAFUNZI mmoja wa utabibu aliuawa kwa kudungwa kisu katika Kaunti ya Trans Nzoia, siku chache kabla ya siku ya sherehe yake ya kufuzu.
Benedict Kiptoo, 24, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Mafunzo ya Utabibu nchini (KMTC), bewa la Kitale alitarajiwa kufuzu Alhamisi Desemba 5.
Hata hivyo, aliuawa kwa kudungwa kisu Jumapili asubuhi baada ya kutofautiana na mpenzi wake wa kike.
Inadaiwa kuwa aliyemshambulia na kumuua Kiptoo ni mhudumu wa mkahawa.
Kulingana na majirani, wawili hao walikuwa wakiishi pamoja katika mtaa wa Kibomet, viungani mwa mji wa Kitale. Hata hivyo, wamekuwa wakigombana kila mara baada ya kutofautiana kuhusu masuala mbalimbali.
Dkt Evans Letting, aliyempa huduma ya kwanza Bw Kiptoo, alisema alikufa baada ya kuvuja damu nyingi.
“Alibisha mlango wangu akiitisha usaidizi lakini alikuwa akivuja damu nyingi zaidi. Tulimkimbiza katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Wamalwa Kijana lakini hakuhudumiwa kwa wakati. Tulilazimika kumkimbiza katika Cherangany Nursing Home lakini alikufa njiani,” Dkt Letting akasema.
Naibu Kamanda wa Polisi Kaunti ya Trans Nzoia Salesio Muriithi alisema mshukiwa wa mauaji hayo alitoroka.
“Tunamsaka. Pindi tutakapomkamata, tutamfungulia mashtaka kwa mujibu wa sheria,” Bw Muriithi akaeleza.
Gladys Kipkorir, ambaye ni mamake marehemu na mkazi wa Sacho, Kaunti ya Baringo, alielezea machungu kufuatia kisa cha kifungua mimba wake.
Familia hiyo iliyojawa majonzi ilisema kuwa haikuwa na habari kuwa mwana wao alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mshukiwa.
“Tunatoa wito kwa polisi kuchukua hatua za haraka na kumkamata mshukiwa. Ninahisi uchungu kama mama na kile ninachotaka ni kupata haki kwa mtoto wangu,” Bi Kipkorir akasema.
Kwa machungu mama huyo alielezea jinsi mwanawe alikuwa alikuwa amechukuaa mavazi ya sherehe ya kuvuzu wiki jaa kutoka Nairobi lakini furaha ya kumwona akifuzu rasmi sasa imekatizwa na mauti.
“Mtoto wangu alikuwa akijiandaa kufuzu Alhamisi wiki hii. Nimempoteza mwanangu wa kiume ambaye alikuwa nguzo katika maisha yangu. Ameenda na hatarejea; sasa kile tunachohitaji ni haki,” Bi Kipkorir akasema.
Mjombake Kiptoo, Japheth Kipkorir alimwelezea mpwa wake kama mtu mbunifu na mwenye bidii ambaye alikuwa na ndoto kuu ya kusaidia familia yake.
“Tulikuwa na matarajio makubwa kutoka kwake. Tumempoteza mtu mwenye ujuzi na bidii na ninashuku kuwa hizo ndizo sifa ambazo msichana huyo aliona kwake,” akasema.
Aliongeza kuwa Kiptoo pia alijihusisha katika biashara ya kuuza bidhaa za urembo na alikuwa na ujuzi wa kusanifu makucha miongoni mwa huduma zingine za urembo.
Mwili wa Kiptoo uko katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Cherangany Nursing Home huku wapelelezi wakiendelea na uchunguzi kuhusu chanzo cha kisa hicho cha mauti.
Hata yanajiri baada ya Waziri wa Afya katika Kaunti ya Trans Nzoia Sam Ojwang kuonya vijana dhidi ya kushiriki katika mahusiano ya kimapenzi yasiyo thabiti kwa sababu yanaweza kusababisha mauti.