Habari za Kitaifa

Wetang’ula ajitetea asirushwe jela 

Na JOSEPH WANGUI April 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SPIKA wa Bunge la Taifa, Moses Wetang’ula, ameiomba mahakama kutupilia mbali kesi ya wanaharakati wanaotaka ajiuzulu na kufungwa jela kwa madai ya kupuuza uamuzi wa mahakama uliotangaza muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya ndio mrengo wa walio wengi Bungeni.

Katika stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani Ijumaa, Aprili 4, 2025 Bw Wetang’ula ameomba kesi ya kudharau korti iliyoanzishwa dhidi yake na kundi la wanaharakati wa kisiasa Februari 2024 itupiliwe mbali.

Kesi hiyo inahusiana na uamuzi wake kuhusu uongozi wa bunge.

Wetang’ula anasema kuwa ana kinga dhidi ya mashtaka ya kudharau korti, na hivyo, kesi kama hiyo haiwezi kufunguliwa dhidi yake kuhusiana na utekelezaji wa majukumu yake rasmi.

Mvutano huu wa kisheria pia unahusu kushikilia wadhifa wake kama kiongozi wa chama cha Ford Kenya na Spika wa Bunge la Taifa kwa wakati mmoja.

Wanaharakati hao, kupitia wakili wao Kibe Mungai, wanataka Wetang’ula afungwe jela kwa miezi sita kwa kukataa kutambua Azimio kuwa mrengo wa walio wengi kinyume na uamuzi wa mahakama.

Hata hivyo, katika ombi jipya, Wetang’ula anasisitiza kuwa mashtaka ya kudharau mahakama dhidi yake yanakiuka mamlaka, haki, na kinga za bunge kama inavyoelewa katika Kifungu cha 117 cha Katiba.

Katika utetezi wake, anasema kuwa kabla ya kesi ya dharau kufunguliwa, walalamishi hawakutoa wala kumkabidhi nakala ya amri rasmi ya mahakama kwake au kwa Bunge la Taifa.

“Walalamishi hawajatoa wala kutoa nakala ya amri ya mahakama kwa Spika au Bunge la Taifa ili kuhalalisha mashtaka haya ya dharau,” anasema wakili wake, Judith Guserwa.

Akitaka kesi hiyo itupiliwe mbali, Wetang’ula anadai kuwa mashtaka hayo yamechanganywa na masuala mengine, na hivyo kuyafanya kukiuka haki yake ya kusikilizwa kwa haki.

Pia, anahoji kuwa mamlaka ya mahakama ya kuadhibu mtu kwa dharau yanahusu tu kutotii amri zake.

Katika kesi hii, anasema hakuna amri au hukumu ya mahakama iliyotolewa Februari 7, 2025 inayoweza kusababisha mashtaka ya dharau.

“Hakuna amri maalum iliyotolewa na mahakama ambayo Spika au Bunge la Taifa wangeweza kukiuka au kutakiwa kutekeleza. Hakuna agizo lolote la mahakama lililotaka Bw Wetang’ula na Bunge kufanya au kutofanya jambo fulani,” anasema.

Bunge la Taifa pia limeunga mkono ombi lake, likisema kuwa kesi hiyo ni jaribio la wanaharakati hao kufufua kesi iliyoamuliwa.