Habari za Kitaifa

Wetangula apuuza msimamo wa Raila, aunga NG-CDF

Na  BENSON MATHEKA August 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, ametofautiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga huku akitetea Hazina ya Maendeleo wa Maeneobunge (NG-CDF).

Bw Wetang’ula alisisitiza kuwa hazina hiyo imechangia pakubwa katika maendeleo ya elimu na miundombinu katika ngazi ya mashinani na kitaifa, licha ya baadhi ya miito ya kutaka ivunjwe.

Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa wabunge hawafai kusimamia hazina hiyo akipendekeza ihamishiwe kwa serikali za kaunti.

Kulingana na Raila hatua hiyo itaboresha ufanisi, kuimarisha ugatuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Katika mfumo huu mpya(ugatuzi), CDF haina maana tena,” alisema Raila awali.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi rasmi wa jengo jipya la madarasa katika Shule ya St. Veronica Ranje R.C. Comprehensive, eneobunge la Kanduyi,Bw Wetang’ula alisema  hazina hiyo imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa zaidi ya miongo miwili.

“NG-CDF  imeleta mabadiliko halisi. Nilipoingia Bungeni mara ya kwanza, haikuwepo. Tangu kuanzishwa kwake, miradi iliyofadhili imebadilisha maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa,” alisema Spika Wetang’ula.

Alisema licha ya mahakama kutangaza hazina hiyo kuwa kinyume cha Katiba, Bunge lilifanya marekebisho ya sheria ili kuifanya kuwa halali kikatiba.

“Matumizi bora ya fedha za umma yanaonyeshwa vyema kupitia miradi ya NG-CDF. Katika kila kijiji, miradi  kama madarasa, maabara au vituo vya afya imefadhiliwa na hazina  hii,” aliongeza Wetang’ula.

Jengo jipya lililozinduliwa linajumuisha madarasa 12 ya kisasa na ofisi za usimamizi zilizo na vifaa kamili. Spika alisifu NG-CDF ya Kanduyi kwa kuwekeza katika miundombinu inayowasaidia walimu na wanafunzi.

“Tulipopeleka Mswada wa kuingiza NG-CDF katika Katiba, asilimia 90 ya wabunge waliuunga mkono. Hii ni kwa sababu Wakenya kote nchini wanatambua mchango wake,” alisema.

Mbunge wa Kanduyi, John Makali, alitaja NG-CDF kama mfano bora wa maendeleo ya mashinani ikilinganishwa na miradi ya serikali za kaunti.

“Tofauti na baadhi ya miradi ya kaunti, uwekezaji wa NG-CDF unaonekana wazi – iwe ni madarasa, maabara au vituo vya afya. Ni mfano wa maendeleo ambayo watu wanaweza kuona na kuthamini,” alisema Makali.

Naye Mbunge wa Webuye Mashariki, Martin Pepela, aliunga mkono kauli hizo na kusifia matumizi bora ya hazina hiyo katika kuboresha mazingira ya wanafunzi na walimu.

Alikosoa pendekezo la kuhamishia hazina hiyo kwa serikali za kaunti au kuifuta kabisa, akisema wale wanaotoa mapendekezo hayo hawajui hali halisi ya maisha mashinani.

“Tunaunga mkono NG-CDF. Kwa wanaopendekeza irejeshwe kwa kaunti, waite kura ya maoni waulize Wakenya kama wanataka ivunjwe. Jibu litakuwa wazi,” alisema Pepela.

Alisisitiza kuwa hazina hiyo imekuwa nguzo muhimu ya kuwezesha shule kupata vifaa na miundombinu inayofanikisha utoaji wa elimu bora nchini.