Habari za Kitaifa

Wetang’ula awataka wabunge waongeze ufadhili kwa sekta ya michezo

Na BENSON MATHEKA December 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang’ula, ametoa wito kwa Wabunge kutenga pesa zaidi kwa Wizara ya Michezo.

Akizungumza katika Kaunti ya Uasin Gishu Jumamosi asubuhi, Spika Wetang’ula alisema kuwa riadha bila shaka ndiyo jukwaa kuu la kuitangaza Kenya kimataifa.

Alisema Wimbo wa Taifa wa Kenya umekuwa ukipigwa katika miji mikuu duniani kutokana na juhudi, ujasiri na moyo wa wanariadha wa Kenya.

Akizungumza wakati wa toleo la tatu la mbio za Great Chepsaita, Wetang’ula alisema Kenya ina vipaji visivyo na mipaka.

“Tuna kila sababu ya kujivunia wanarika wetu wanaposhinda mbio katika uwanja wa kimataifa. Kila mara ninapoona vijana wetu wakibeba taifa letu nje ya nchi, naona fahari zaidi kama Mkenya,” alisema.

Hafla  hiyo ya kila mwaka huandaliwa na Farouk Kibet, Msaidizi wa Rais William Ruto.

Wetang’ula alimsifu Farouk kwa juhudi za kukuza vipaji katika makundi ya kila umri.

“Katika wadhifa wangu kama Spika wa Bunge la Taifa, nawahimiza Wabunge kutenga rasilimali zaidi kwa michezo ili kukuza vipaji. Nimejitolea kuunga mkono shughuli zote za michezo,” alisema.

Spika Moses Wetang’u;la na baadhi ya washindi wa mbio za Chepsaita Kaunti ya Uasin Gishu mwaka wa 2025

Alisisitiza pia umuhimu wa umoja:“Lazima tupendane na kumuunga mkono Rais Ruto na Serikali yake ili kuhakikisha uongozi unatimiza ndoto yake. Vipaji vyetu havina mipaka na vitatupeleka mahali tunapostahili kuwa. Sote tunastahili kujivunia utaifa wetu.”

Gavana wa eneo hilo, Jonathan Bii, alisema serikali yake itaendelea kuunga mkono shughuli za michezo.

“Tumeona vijana wakishiriki michezo mbalimbali. Ni heshima kuwa nao, na tunajivunia mustakabali wa michezo katika nchi yetu,” alisema Bii.

Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa, alisema ataanzisha toleo lingine la mashindano hayo ili kuendeleza vipaji kote nchini.

“Mwandalizi ametupa mfano; sisi tutafuata. Hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya michezo nchini,” aliongeza.

Katibu wa Elimu ya Msingi, Prof Julius Bitok, alisema hafla hiyo inaendelea kukuza vipaji nchini kote.

“Serikali imefanya mengi katika sekta ya elimu. Nimefurahia kwamba hafla ya leo imeandaliwa mahsusi kuunga mkono masuala ya elimu,” alisema Prof Bitok.

Bingwa wa dunia wa riadha, Paul Tergat, alisema tukio hilo linawapa motisha wale wanaotaka kujipatia riziki kupitia michezo.

“Tutakuwa na vipaji vingi zaidi siku zijazo. Wadau wote wanapaswa kukumbatia wazo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika michezo,” alisema Tergat.

Mwakilishi wa Wanawake wa Nandi, Muge Cynthia, alitoa wito kwa viongozi zaidi kushiriki katika shughuli za michezo.

“Tunajivunia kuwa taifa linalotambulika duniani kwa sababu ya vipaji vyetu. Sisi sote lazima tushirikiane ili tusipoteze hazina hii kubwa,” alisema