Wetang’ula kuwakilisha Afrika katika Jumuiya ya Madola
NA BENSON MATHEKA
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amechaguliwa kwa mhula wa pili kuwa mwakilishi wa Afrika katika Kamati ya Kudumu ya Kongamano la Maspika wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola (CSPOC).
Spika Wetang’ula aliteuliwa bila kupigwa kuhudumu kwa muhula wa pili katika kamati ya shirika hilo katika uchaguzi uliofanyika Kampala, Uganda.
Kanda ya Afrika ina wawakilishi watatu katika CSPOC na Bw Wetang’ula atawakilisha Afrika pamoja na Spika wa Ghana na Spika wa Ufalme wa Eswatini.
Spika wa Uganda anabakia kuwa Mwenyekiti kwa sababu ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu, 2024, ilivyoainishwa katika kanuni za CSPOC kwamba Spika mwenyeji anaendelea kuwa mjumbe.
Kamati ya Kudumu ya CSPOC ina jukumu la kupendekeza ajenda ya kujadiliwa katika mkutano ujao; kupitia sheria za kudumu na kuzingatia masuala ya kifedha ya CSPOC; na kuamua tarehe, maeneo na taratibu za mkutano ujao.
Katika mkutano huo, washiriki walijadili masuala ibuka yanayoathiri Bara la Afrika hususan athari za mabadiliko ya tabianchi, sheria zinazoathiri makundi ya Afrika, umoja wa Afrika pamoja na uteuzi wa Wawakilishi wa Afrika kwenye Kamati ya Kudumu ya CSPOC.
Akizungumza Alhamisi, Januari 4, 2024 wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamano la 27 la Maspika wa Jumuiya ya Madola (CSPOC), Bw Wetangula alisema kuwa majanga yanayohusiana na hali ya hewa yanazidi kutokea mara kwa mara na kuwa makali na kuzuia juhudi za kuangamiza umaskini Barani Afrika.
“Nchi za Jumuiya ya Madola, hasa zile za kusini mwa dunia, ndizo zinazokabiliwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa mazingira licha ya kuchangia kidogo hali hiyo,” alisema Spika Wetang’ula.
Wetang’ula alisisitiza kuwa Afrika inaathiriwa zaidi kuliko kanda nyingine na mabadiliko ya hali ya hewa licha ya mchango wa bara hilo kuwa chini ya asilimia nne ya jumla ya uzalishaji wa gesi chafu.
Spika Wetang’ula pia alieleza wasiwasi kwamba nchi za Afrika zinapaswa kutumia mapato yake katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo, ambayo kwa sasa inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya Pato la Taifa kila mwaka kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.