Wingu jeusi lagubika Kenya ‘Baba wa Haki na Demokrasia’ akifariki dunia
MSHTUKO wa kwanza kwa Wakenya jana asubuhi zilikuwa habari kuhusu kifo cha kinara wa ODM, Raila Amolo Odinga.
Lakini mshtuko wa pili, wa kimya na wa kushangaza zaidi, ulijitokeza saa chache baadaye: Kwamba, kwa mujibu wa jamaa wa karibu wa familia na maafisa wa Ikulu wanaoshughulikia mipango ya mazishi, Bw Odinga aliacha agizo mahsusi akitaka azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.
Kwa hivyo, kwa mujibu wa mipango ya sasa, mazishi ya kitaifa ya kiongozi huyo huenda yakafanyika mwishoni mwa juma hili.
Matakwa haya ya mwisho ya Bw Odinga yalifichuliwa na wakili wake katika kikao kilichofanyika Ikulu Jumatano asubuhi, kikao kilichohudhuriwa na kaka yake, Seneta Oburu Oginga.
Hata hivyo, changamoto kubwa imeibuka kuhusu lini saa 72 zinafaa kuanza kuhesabiwa ikiwa ni kuanzia wakati wa kifo au baada ya mwili kufikishwa nchini.
Baadhi ya walio kwenye kamati ya maandalizi wanapendekeza saa zianze kuhesabiwa mwili utakapowasili nchini, lakini wengine wanaamini hilo litakuwa kinyume cha matakwa ya marehemu, na kwamba, agizo lake linahitaji kutekelezwa bila kuchelewa.
Jana jioni, afisa mmoja kutoka Wizara ya Masuala ya Kigeni alidokeza kuwa mwili wa Bw Odinga unatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi jioni, saa chache kabla ya saa 72 kukamilika.

Safari ya ndege kutoka Mumbai, India hadi Nairobi huchukua takriban saa sita na dakika kumi na tano.
Kwa mujibu wa duru za karibu, ilikuwa Seneta Oburu Oginga aliyempigia Rais William Ruto saa moja asubuhi akimjulisha kuwa ndugu yake mdogo alikuwa katika hali mahututi hospitalini Mumbai.
“Alisema Raila alikuwa amerudishwa hospitalini kwa dharura,” duru zetu zilisema.
Dakika chache baadaye, simu nyingine iliingia. Safari hii ilikuwa kutoka kwa binti wa Bw Odinga, Bi Winnie Odinga, aliyempigia Rais Ruto moja kwa moja.
“Alizungumza kwa kifupi, sauti yake ikitetemeka. Alithibitisha kuwa jambo baya zaidi limetokea,” duru hizo ziliongeza.
Kifo cha Raila kilizua huzuni nchini kote wafuasi wake wakimlilia kwa machozi na nyimbo za maombolezo.
Raila Odinga, 80, alifariki dunia Jumatano asubuhi Koothattukulam, wilayani Ernakulam nchini India, baada ya kupata mshtuko wa moyo akifanya matembezi yake ya kila asubuhi, kulingana na polisi na viongozi wa hospitali.
Odinga alikimbizwa hospitali Koothattukulam, ambapo alitangazwa kuwa amefariki dunia.
Habari za kifo chake zilisababisha huzuni huku maelfu ya Wakenya wakiingia barabarani kwa pikipiki, magari na miguu wakibeba matawi ya miti na kupiga honi kwa vilio na nyimbo za maombolezo katika kaunti za Nairobi Kisumu, Siaya, Homa Bay, Migori, Kakamega na Kisii na Machakos.
Katika kaunti ya Siaya, nyumbani kwa marehemu, vijana walifunga Barabara ya Bondo-Kisumu huku wakiimba na kulia, wakisema kwa lugha ya Dholuo: “Ng’ou olwar jokamaa” — yaani “Mti mkubwa umeanguka.”
Wazee wa jamii ya Sakwa walikusanyika nyumbani kwa Raila huko Opoda, Bondo, wakiomboleza kwa kulia waziwazi, wengine wakizunguka nyumba yake kwa vilio vya kitamaduni.
“Maumivu haya ni makali mno. Kwa nini kifo kije wakati huu kutuondolea mwana wetu shujaa?” alihoji John Odira, mzee kutoka Sakwa.
“Huyu alikuwa mfalme wetu na shujaa wa eneo hili.”
Katika jiji la Kisumu, biashara nyingi zilifungwa kufikia saa nne na nusu asubuhi. Wakazi walimiminika barabarani wakibeba bendera za Kenya, matawi ya miti na leso, huku nyimbo za huzuni zikitawala anga.
“Sisi kama taifa tupo njia panda,” alisema John Otieno, mmoja wa waombolezaji.
“Tuna wasiwasi ikiwa uhuru na haki alizotupigania zitaendelea.”
Rosemary Adhiambo, ambaye alikuwa akilia kwa uchungu, alisema: “Siasa ya Kenya haieleweki bila Raila. Hakuna wa kujaza nafasi yake kwa sasa.”
Baraza la Wazee wa Jamii ya Luo, likiongozwa na Ker Odungi Randa, liliwaomba magavana wanne wa Nyanza — James Orengo (Siaya), Prof Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Gladys Wanga (Homa Bay) na Ochilo Ayacko (Migori) — kuongoza jamii kwa amani wakati huu mgumu.
“Leo nimehisi uchungu sana. Wakati Jaramogi alikufa sikulia, lakini leo Raila alipokufa nimelia,” alisema Ker Randa akiwa katika Ukumbi wa Ofafa Memorial.
Mjini Homa Bay, maelfu ya wananchi walifanya gwaride la kijadi la Tero Buru, wakisindikiza ng’ombe mbele yao kama ishara ya kumuenzi mtu mkubwa aliyefariki.
Baadhi walibeba mashoka, mikuki na mishale, ishara za jadi za kulinda jamii dhidi ya maafa.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Homa Bay, Polycarp Okombo, aliongoza wajumbe na viongozi katika kusimamisha vikao vyao rasmi kwa heshima ya marehemu.
Mjini Kisii, wanafunzi wa Kisii National Polytechnic walitoka kwenye vyumba vya mitihani na kuelekea barabarani kuomboleza kifo cha Raila. Wakiimba na kubeba matawi, walizunguka mji wakimsifu kama “Baba wa taifa.”
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa taifa,” alisema Hellen Nyamweya, kijana kutoka Kisii. “Tutamkosa sana.”
Katika eneo la Magharibi, baadhi ya viongozi walisitisha shughuli zao kwa heshima ya marehemu.
Katika jiji la Nairobi wakazi walifika katika boma la Raila mtaani Karen na kuingia barabarani wakiomboleza.
Vilio vilisikika katikati ya jiji huku baadhi ya biashara zikifungwa kwa hofu.
Kwa kilio cha huzuni, wakazi wa mtaa wa Kibera, inayofahamika kama ‘bedroom’ ya Raila, waliingia katika barabara ya Ngong na baadhi wakatembea hadi Karen kuthibitisha habari za kifo chake wakilalamika kutofahamishwa awali ukweli kuhusu hali yake ya afya.