• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Wito basi la bima ya lori liendelee kushikiliwa na polisi

Wito basi la bima ya lori liendelee kushikiliwa na polisi

NA SAMMY KIMATU

CHAMA cha madereva wa malori ya masafa marefu (LoDDCA) kimeiomba serikali kutoruhusu basi lililohusika katika ajali ya barabarani iliyoua watu 15 kuondolewa katika kituo cha polisi cha Nakuru.

Afisa Mkuu Mtendaji wa LoDDCA Anthony Mutua kupitia barua kwa vyombo vya habari, alisema amesikitishwa sana na ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la Classic Kings of Congo na matatu.

“Rambirambi zetu za dhati zinaenda kwa familia zilizoathiriwa na tunaendelea kujitolea katika kukumbatia sheria za usalama barabarani na kutafuta haki kwa wanachama wetu na umma kwa ujumla,” Bw Mutua alisema.

Bw Mutua alisema kuna dalili za kutisha kwamba usimamizi wa Classic unazingatia kuvuruga ushahidi muhimu kuhusiana na kesi inayoendelea.

Soma Pia: Kumbe basi lililoua abiria 15 lilikuwa na bima ya lori!

Aliongeza kuwa kampuni ya mabasi ya Classic inadaiwa kuwa na mpango wa kuondoa mabaki ya basi hilo mikononi mwa polisi, hivyo kuibua wasiwasi wa uwezekano wa kuficha taarifa muhimu kwa ajili ya uchunguzi.

“LoDDCA ingependa kusisitiza kwamba Kampuni ya Mabasi, wakati wa utendakazi wake, imekiuka vifungu vingi vya Sheria za Trafiki na Kanuni za Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA),” barua hiyo ilisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tuhuma dhidi ya kampuni hiyo ni pamoja na uendeshaji wa mabasi ambayo kiufundi hayako sawa, kwa hiyo, yanachukuliwa kuwa hayafai kuwa barabarani.

Alibainisha ukiukaji wa pili ni kutofuata sheria za NTSA za kuwa na madereva wawili kwenye safari za masafa marefu.

LoDDCA ilisema wanafahamu kuwa kesi hiyo imewasilishwa rasmi katika mahakama ya Molo na dereva wa basi lililoharibika pia alikamatwa.

Aliongeza kuwa dereva huyo kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi huku uchunguzi ukiendelea.

Bw Mutua alikariri kuwa LoDDCA inatoa wito kwa haraka kutaka polisi kukataa jaribio lolote la kuachilia basi hilo lililokumbwa na misukosuko hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa mahakamani.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Tutatuma vijana milioni moja ng’ambo mwaka huu – Moses...

Safaricom yaomba radhi huduma ya PayBill ikikumbwa na...

T L