Wito fedha za NG-CDF zimwagwe kwa miradi ya kubuni ajira
NA LAWRENCE ONGARO
WATAALAMU wamekosoa mtindo wa wanasiasa kutumia fedha za hazina ya maendeleo ya maeneobunge (NG-CDF) kwa namna ambayo haisaidii kivyovyote vile katika kubuni nafasi za kazi kwa vijana.
Wkichangia suala hilo, walishangaa kuwa hata wanafunzi wa viwango vya uzamifu na uzamili hutarajia kupokea fedha hizo za NG-CDF.
“Ni jambo la kushangaza kuona msomi wa kiwango hicho akionyesha hundi ya fedha za NG-CDF. Hii kwetu ni aibu,” alisema Katibu wa Maswala ya Mawasiliano katika Ofisi kuu ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Maliba Arnold Nyajayi.
Alisema hata ingawa fedha za NG-CDF mara nyingi huwafaa sana wanafunzi walioko katika shule za upili, ni vyema pia kiasi kikubwa cha fedha kuelekezwa katika maendeleo yanayohusu ujenzi wa miundomsingi ili kuwapa vijana kazi.
Lakini pia katika elimu, alisema fedha hizo huchirizwa kidogo mno, akisema baadhi ya wanafunzi hupokea kati ya Sh500 na Sh5,000 kiasi alichosema ni kidogo mno.
Mwenyekiti wa miungano ya vyuo vyote vikuu vya kibinafsi Vincent Gaitho alisema wazazi wengi wanapitia changamoto ndipo wapate mgao kwa manufaa ya watoto wao.
“Wazazi wengi kutoka maeneo ya miundomsingi duni na mazingira magumu, wanapitia changamoto kubwa ya kunufaika na fedha hizo za NG-CDF,” alifafanua Dkt Gaitho.
Alisema kwa muda wa miezi saba hivi kumekuwepo na kucheleweshwa kwa usambazaji wa fedha hizo.
“Wengi wa viongozi hasa wabunge hutumia fedha hizo kujinufaisha kisiasa jambo linaloleta utata,” alisema Dkt Gaitho.
Kinara huyo alitoa wito kwa viongozi wakipewa majukumu ya kusambaza fedha hizo wafanye juhudi kuona ya kwamba maendeleo ya kunufaisha jamii yanatekelezwa mara moja.
Alisema kila eneobunge lina matakwa yake ya kimaendeleo na kwa hivyo wawe makini wanaposambaza fedha hizo.
Aliwashauri wakulima wasiharibu chakula wakati wa mavuno mengi.
Alitaja mahindi, maziwa, maembe na hata mboga kama mazao muhimu vijijini.
Alipongeza mradi maalum wa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro akisema amefanya maajabu.
Kati ya shule 20 za kutwa zimesimamiwa kwa kila kitu ila tu wanalipia fedha za karo ya Sh1,000 pekee kwa kila mzazi.
Dkt Gaitho alitoa wito kwa wanafunzi waliopata chini ya alama C+ kujiandaa kujiunga na shule za kiufundi za TVET ili wapate ujuzi zaidi wanapokamilisha masomo hayo ya kiufundi.