• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Wito jamii ya kimataifa ilazimishe kufutiliwa mbali mkataba kati ya Ethiopia na Somaliland

Wito jamii ya kimataifa ilazimishe kufutiliwa mbali mkataba kati ya Ethiopia na Somaliland

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wanne kutoka eneo la Kaskazini Mashariki wameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati na kushinikiza kufutiliwa mbali mkataba unaoipa Ethiopia kibali cha  kutumia eneo karibu na bandari ya Berbera iliyo eneo linalopania kujitenga la Somaliland.

Kulingana na mkataba huo uliotiwa saini jijini Addis Ababa, Ethiopia, Jumatatu, Ethiopia itatumia eneo la upana wa kilomita 20 karibu na bandari ya Berbera kwa shughuli za wanajeshi wake wa majini na shughuli za kibiashara.

Mkataba huo ambao utadumu kwa miaka 50 ulitiwa saini kwa pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kiongozi wa Somaliland Muse Bihi Abdi.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amepinga mkataba huo akisema ni hatari na kwamba ni sawa na Ethiopia kuingilia himaya ya Somalia.

Rais Mohamud anashikilia kuwa eneo la Somaliland liko chini ya serikali ya taifa la Somalia, japo limekuwa likitaka kujitenga.

Nao wabunge hao wa Kenya, wakiongozwa na Farah Maalim (Daadab), wanasema Somaliland haina mamlaka ya kukodisha eneo la karibu na bandari hiyo ya Berbera kwa Ethiopia.

“Tunatoa wito kwa Umoja wa Afrika (AU), Shirika la Maendeleo la IGAD na Umoja wa Mataifa (UN) kuingilia kati na kuzuia Ethiopia kutwaa eneo lililoko ndani ya himaya ya Somalia kinyume cha sheria,” Bw Maalim akasema Alhamisi kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Mkataba kama huo unaweza kuleta vita kati ya Ethiopia na Somalia na athari zake zinaweza kufika Kenya ikizingatiwa sisi ni majirani. Isitoshe, jamii za Kaskazini Mashariki zina uhusiano wa kiukoo na jamii za Somalia na Ethiopia,” akaongeza Bw Maalim ambaye ni Naibu Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa.

Alikuwa ameandamana na Mbunge wa Eldas Aden Keynan, Yakub Hassan (Fafi), na Abdikadir Hussein Mohamud wa Lagdera.

Kulingana na mkataba huo, Ethiopia ingetumia eneo hilo la bandari na kisha itambue Somaliland kama taifa huru.

  • Tags

You can share this post!

Tusipolinda mazingira tunaalika umaskini, Wetang’ula aonya

Mbolea nafuu iliyohepeshwa yaanikwa kama ushahidi dhidi ya...

T L