Habari za Kitaifa

Wito ‘Sheria za Matiang’i’ zizingatiwe kupunguza ajali

March 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

ONGEZEKO la ajali za barabarani zinazohusisha mabasi ya shule, limezua hofu miongoni mwa wadau wa elimu nchini, ambapo sasa wanasema kuwa chanzo chake kikuu ni kutozingatiwa kwa kanuni zilizowekwa na Waziri wa Elimu wa zamani, Dkt Fred Matiang’i.

Baadhi ya shule na vyuo ambavyo mabasi yao yamehusika katika ajali katika siku za hivi karibuni ni Shule ya Upili ya Wavulana na Kapsabet, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Chuo Kikuu cha Moi kati ya taasisi nyingine.

Mnamo Machi 16, 2024, watu wawili—mwalimu na mwanafunzi—waliaga dunia baada ya basi la Shule ya Upili ya Wavulana ya Kapsabet kuanguka katika eneo la Patkawanin, kwenye barabara ya Kabarnet-Marigat.

Wanafunzi wengine zaidi ya 50 walijeruhiwa kwenye ajali hiyo.

Mnamo Machi 18, 2024—siku mbili tu baada ya ajali ya Shue ya Upili ya Wavulana ya Kabarnet—wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walifariki kwenye ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika eneo la Mackinnon, kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Ajali hiyo ilitokea baada ya basi la shule hiyo kugongana ana kwa ana na trela.

Mnamo Jumatano, wanafunzi 12 wa Chuo Kikuu cha Moi walipata majeraha, baada ya basi lao kuhusika kwenye ajali katika eneo la Kimende, kwenye barabara ya Nairobi-Nakuru.

Kufuatia tukio hilo, chuo hicho kilitangaza kusimamisha ziara zote za kimasomo.

Kutokana na mkondo huo wa kuhofisha, wataalamu wa masuala ya kielimu wanasema kuna uwezekano visa hivyo vinachangiwa na taasisi hizo kutozingatia kanuni zilizowekwa na Dkt Matiang’i.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, aliyekuwa Waziri wa Elimu katika Kaunti ya Nairobi, Bi Muthoni Ouko, anasema kuwa wakati umefika shule kutathmini utekelezaji mpya wa kanuni hizo.

“Moja ya masharti ambayo Dkt Matiang’i aliweka ni ni kuwa wanafunzi hawafai kusafiri baada ya saa 12 jioni. Hata hivyo, inasikitsha kuwa katika baadhi ya shule, walimu na wanafunzi wamekuwa wakisafiri nyakati za usiku, hali ambayo inahatarisha maisha ya wasomi hao wachanga,” akasema.

Pia, anasema baadhi ya shule zimekuwa zikiyakodisha mabasi yao kwa watu tofauti kuhudhuria hafla mbalimbali, ambapo usimamizi wa shule hizo huwa hautilii mkazo mabasi hayo kuchunguzwa kuhusu ikiwa yana hitilafu zozote za kimitambo.

“Dkt Matiang’i pia alizizuia shule dhidi ya kuyakodisha mabasi au magari yake kutumika katika hafla tofauti.  Hili ni kuhakikisha kuwa magari hayo hayatumiki visivyo. Hata hivyo, agizo hilo limekuwa likikiukwa,” akasema.

Kulingana na Dkt Emmanuel Manyasa, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu, ni vizuri taasisi za elimu zianze kutathmini baadhi ya kanuni hizo, ili kuhakiksha wanafunzi hawana wasiwasi wowote wanapoenda kwenye ziara za kielimu.

“Visa hivi vya ajali bila shaka huwa vinawaathiri wanafunzi kisaikolojia. Ni hali inayoweza kuwatia hofu wanafunzi, kiasi kwamba baadhi yao wanaweza kudinda kushiriki kwenye ziara za kielimu katika siku za usoni,” akasema Dkt Manyasa.