• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Wizara yatoa onyo la mafuriko mabwawa ya Masinga, Kindaruma yakivunja kingo

Wizara yatoa onyo la mafuriko mabwawa ya Masinga, Kindaruma yakivunja kingo

Na WAANDISHI WETU

WIZARA ya Usalama wa Ndani imetoa ilani kuhusu uwezekano wa mafuriko zaidi kutokea katika sehemu mbalimbali nchini baada ya mabwawa makuu nchini kuvunja kingo huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha kote nchini.

Kufikia Jumatano asubuhi, mabwawa ya Seven Forks yanayozalisha nishati ya umeme yalikuwa yamejaa pomoni huku Bwawa la Masinga, ambalo ndilo kubwa zaidi, likibubujika maji na kujaza mabwawa mengine.

Kupitia taarifa aliyotumwa jana, Waziri Kithure Kindiki alisema japo kufurika kwa Bwawa la Masinga hakutaathiri kwa sasa mabwawa ya Kamburu, Gitaru, Kindaruma na Kiambere, maeneo yenye makazi ya watu katika bwawa la mwisho la Kiambere yapo hatarini.

Katika eneo la Pwani na Kaskazini, Kaunti za Garissa, Lamu na Tana huenda zikakumbwa na mafuriko endapo Mto Tana na Mto Thiba itavunja kingo kutokana na mvua inayonyesha.

Watu wanaoishi karibu na Ziwa Victoria na mito katika Kaunti za Homa Bay, Siaya, Busia, Kisumu, Migori, Kakamega na Vihiga vilevile wanakodolea macho janga la mafuriko.

Aidha, mafuriko hayo yanatazamiwa kuathiri maeneo ya nyanda za chini zikiwemo Kaunti za Narok, Kajiado na Mombasa pamoja na kaunti zilizopo milimani zinazoathiriwa na maporomoko ya ardhi kama vile Makueni, Nyeri, Murang’a na Pokot Magharibi.

Maeneo ya mijini vilevile hayatanusurika janga la mafuriko kutokana na mifereji duni ya kupitishia maji au iliyoziba huku mabwawa ya umma na ya kibinafsi nchini yakitarajiwa kufurika ikiwa mvua zitaendelea kunyesha.

“Tishio la mafuriko katika sehemu mbalimbali nchini limefanya serikali kumakinika zaidi. Umma umefahamishwa kujihadhari, kupanga safari zao na kujiepusha na tabia hatari kwenye maji yanayosonga,” alisema Profesa Kindiki.

Waziri Kindiki alisema “serikali imechukua hatua za kuhakikisha ulinzi na usalama wa umma na imejiandaa kuzuia athari zote mbaya za mafuriko nchini.”

Katika kaunti ya Kirinyaga, mwanamke alikufa maji baada ya kusombwa na mafuriko akivuka Mto Gakungu, Kaunti Ndogo ya Mwea Magharibi.

Katika Kaunti ya Homa Bay, watu 1,731 wanaishi katika kambi za muda baada ya kufurushwa makwao na maji ya mafuriko.

Kamishna wa kaunti, Moses Lilan, alisema mafuriko yameharibu ekari 350 za ardhi katika kaunti hiyo huku maeneo yaliyoathiriwa pakubwa yakiwa Simbi, Kobuya, Chuowe na Osodo katika Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Kaskazini.

Kamishna huyo alisema mafuriko pia yameathiri familia katika eneo la Ndhiwa na Kisiwa cha Remba.

Katika Kaunti ya Nairobi, mafuriko yameathiri kampuni kadhaa eneo la Viwandani kufuatia matukio ya unyakuzi wa ardhi katika kingo za Mto Ngong.

Manaibu Makamishna wa Kaunti ya Makadara na Starehe, Mabw Philiph Koima na John Kisang, walisema kuwa kingo za Mto Ngong zilivamiwa na watu walafi ambao wamejenga nyumba za kukodisha.

Na Mary Wangari, George Munene, George Odiwuor Na Sammy Kimatu

  • Tags

You can share this post!

Nakhumicha ataka hospitali zikubali NHIF akisema madeni...

Wenger asema Arsenal wana uwezo wa asilimia 50 kushinda...

T L