Wizara yazindua mpango wa kukabili vifo vya watoto wachanga
WIZARA ya afya imeimarisha juhudi za kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini baada ya kuzindua mwongozo mpya kuhusu utunzaji wa watoto wachanga.
Mwongozo huo unadhamiriwa kuwapa wahudumu wa afya ujuzi wa kuwatunza watoto hasa wanapozaliwa kabla ya wakati (miezi tisa).
Waziri wa Afya, Deborah Barasa, Mkurugenzi wa Afya Patrick Amoth na Gavana Gladys Wanga, jana walizindua rasmi vifaa na mwongozo kuhusu jinsi ya kuwatunza watoto wachanga katika Chuo cha Mafunzo ya Matibabu (KMTC) Homa Bay.
Dkt Barasa alisema kuzaliwa kabla ya wakati ndicho kiini cha vifo vya watoto wachanga nchini huku takwimu zikiashiria kiwango cha vifo vya watoto wachanga kuwa 21 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai.
“Takwimu hizo hazijabadilika tangu 2014. Vifo vya watoto wachanga vinachangia asilimia 51 ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano nchini ilhali sehemu kubwa inaweza kuzuiwa kupitia mikakati ya bei nafuu iliyothibitishwa,” alisema.