Yabainika idadi kubwa ya vyama vya kisiasa vimeundwa kutegea ‘kughula’
IDADI kubwa ya vyama 91 vya siasa vilivyosajiliwa nchini vinakabiliwa na hatari ya kufungiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27 na hata chaguzi zijazo kwa kushindwa kutimiza masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2011.
Hii inaibua maswali iwapo vinastahili kufaidika na Hazina ya Vyama vya Siasa.
Hali hiyo imefichuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu, katika ripoti yake ya ukaguzi kuhusu matumizi ya fedha za serikali ya kitaifa kwa mwaka wa kifedha wa 2023/24 iliyowasilishwa bungeni.
Bi Gathungu amelaumu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa (ORPP) kwa kushindwa kuhakikisha vyama vya siasa vilivyosajiliwa vinatii sheria.
Ingawa sheria inasisitiza kuwa chama cha siasa lazima kiwe na afisi halisi katika angalau nusu ya kaunti 47 ili kipate hadhi ya “kusajiliwa kikamilifu”, ripoti ya ukaguzi imebaini kuwa vyama vingi havijatimiza sharti hilo.
Ukaguzi wa kumbukumbu za usajili wa vyama vya siasa katika ORPP umeonyesha kutokuwepo kwa uwiano kati ya taarifa zilizowasilishwa wakati wa usajili na hali halisi ya kuwepo kwa afisi za vyama hivyo, hali iliyosababisha msukumo wa kuvitaka kutii sheria au viondolewe kwenye sajili.
“Ingawa vyama vilitoa anwani za makao makuu na afisi za kaunti kabla ya kusajiliwa, ziara za ukaguzi zilizofanyika Machi 2024 zilionyesha kuwa, idadi kubwa ya vyama hivyo havikuwa na afisi katika zaidi ya nusu ya kaunti,” inasema ripoti hiyo ya ukaguzi.
Ili kuepusha vyama kufungiwa kuwateua wagombea kwenye chaguzi zijazo, Msajili amesema ameanza kuimarisha uwezo wa vyama hivyo kukabiliana na changamoto zilizobainika katika ripoti hiyo ya ukaguzi na masuala mengine ya kifedha.
“Tunafanya ukaguzi mara kwa mara kwa vyama vya siasa vilivyopokea maoni hasi kwenye ukaguzi. Pia tunatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi wa vyama kuhusu usimamizi wa fedha za umma na taratibu zingine zote za vyama,” alisema Bi Sophia Sitati, Kaimu Msajili wa Vyama vya Siasa.
Mbali na vyama 91 vilivyosajiliwa kikamilifu, kumbukumbu za ORPP zinaonyesha kuwa vyama vingine 19 vimesajiliwa kwa muda na vinaendelea kuelekea kupata usajili kamili.
Wachanganuzi wa siasa wanasema vingi huwa vinatumiwa kunufaisha waanzilishi wakati wa uchaguzi kupitia ada za usajili huku wengine wakilenga kuviuza bahati ikiwaangukia.
“Biashara ya vyama vya kisiasa huwa inanoga wakati uchaguzi ukikaribia na kisha waanzilishi na maafisa wanasahau kuna masharti ya kutimiza,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Kulingana na sheria, chama cha siasa kilichosajiliwa kwa muda kinahitimu kusajiliwa kikamilifu iwapo kitawasilisha kwa Msajili maeneo na anwani za afisi zake za matawi, ambazo lazima ziwe zaidi ya nusu ya kaunti zote.
Uchunguzi huru uliofanywa na gazeti hili katika ORPP umebaini kuwa ni vyama vitatu pekee chama cha UDA cha Rais William Ruto, ODM cha Bw Raila Odinga na Wiper cha Bw Kalonzo Musyoka vilivyotii kikamilifu sheria kikamilifu
Ukaguzi huo ulifanyika kabla ya chama kipya cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kusajiliwa kikamilifu.
Ripoti ya ukaguzi imeeleza kuwa vyama vya siasa vinahusisha kutotii sheria kwa ukosefu wa ufadhili wa kutosha kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Siasa, wakilalamikia ugumu wa kulipa kodi za afisi na mishahara ya wafanyakazi baada ya kusajiliwa.
“Hii inazua wasiwasi kuhusu uwezo wa vyama hivyo kuendesha shughuli zao ipasavyo na kuwasiliana na wananchi kote nchini. Katika hali kama hizi, ORPP imekiuka sheria,” inasema ripoti hiyo.