Yabainika wazazi wanakarabati alama za KCPE za watoto wao ndio wapate basari
NA SIAGO CECE
SERIKALI ya Kaunti ya Kwale, imewaonya wazazi waliobadilisha alama ambazo watoto wao walipata kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) wakiwa na lengo la kufaidika na basari ambazo kaunti huwapa wale waliopita mitihani, kwamba hatua hiyo ni ya kihalifu.
Akiongea wakati wa kutoa hundi ya jumla ya Sh35 milioni kwa wanafunzi 923 wanaojiunga na Kidato cha Kwanza, Gavana Fatuma Achani alisema kulikuwa na ongezeko la visa vya baadhi ya wazazi ambao walijaribu kubadilisha alama ili watoto wao wafuzu kwa ufadhili wa masomo.
“Baadhi ya wazazi waliandika 350 katika fomu ilhali wanafunzi walikuwa wamepata alama 300. Hii ni ukiukaji wa sheria na inakuza uvivu miongoni mwa wanafunzi wa kutofanya kazi kwa bidii,” Bi Achani alisema.
Wanafunzi wote wanaopata alama 350 kutoka shule za umma na alama 370 kutoka shule za kibinafsi kwa kawaida huhitimu kupata fedha hizo, huku kipaumbele kikitolewa kwa wahitaji zaidi.
Wazazi wa wanafunzi waliohitimu kwa msaada huo wa fedha wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti hiyo kusambaza hundi za basari chini ya mpango wa kaunti wa Elimu ni Sasa.
Wengi ni wale wanaojiungwa na shule za kitaifa, na watalipwa karo zao hadi watakapomaliza shule ya upili baada ya miaka minne.
Wanafunzi karibu 4,300 kwa sasa wanafadhiliwa na kitita cha Sh500 milioni katika shule mbalimbali za kitaifa kote nchini, huku idadi yao ikitarajiwa kuongezeka katika miaka ijayo.
Bi Achani aliwaambia wazazi kuwa mzigo wao umepunguzwa kwani watahitajika tu kununua sare za shule na mahitaji mengine ya kimsingi kwa watoto wao kabla ya kuripoti shuleni.
“Tunatanguliza elimu kwa sababu tunataka wakazi wetu wote wapate elimu bora kama ilivyo katika mikoa mingine,” Bi Achani alisema.
Zeinab Ismael, mmoja ya wanafunzi ambaye alipata alama 405 na atajiunga na Shule ya Upili ya Kenya High alikuwa miongoni mwa waliofaidika na kusema alijitahidi sana kutokosa fursa hiyo.
“Mradi huu ulinipa motisha ya kusoma kwa bidii na nina furaha nilipata alama za juu na kufuzu kwa ufadhili huo. Hii ni afueni kubwa kwa wazazi wangu kwa sababu hawatalazimika kulipa pesa zozote katika masomo yangu ya shule ya upili,” alisema.
Mpango huo ulizinduliwa mwaka wa 2013, ambapo kila mwanafunzi akipata alama 350 na zaidi anapata usfadhili kamili katika shule ya upili.
Wengi wa wanufaika wamejiandikisha katika shule za kitaifa kote nchini Kenya.