Yafichuka kumbe kuna wabunge huiba marupurupu ya usiku ya walinzi na madereva wao
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amewaonya wabunge kukoma kutia mfukoni marupurupu ya usiku yanayolipwa walinzi na madereva wao akisema tabia hiyo imewachafulia jina bungeni.
Katika warsha ya bunge la kitaifa iliyokamilika majuzi Naivasha, Spika Wetang’ula alisema bayana kwamba “kuiba” hela zinazodhamiriwa walinzi na madereva ni tabia mbovu kwa mtu anayelipwa mshahara na marupurupu ya mamilioni kila mwezi.
“Hebu tafakari mlinzi wako akikuita mwizi na uliiba hela zake kwa miaka yote mitano,” alisema Spika Wetang’ula.
Spika Wetang’ula ndiye mwenyekiti wa Tume ya Huduma ya Bunge (PSC) inayosimamia maslahi ya wabunge na wafanyakazi wa bunge.
Kila mlinzi na dereva wa mbunge ametengewa Sh4,200 kama marupurupu ya usiku hasa wakati mbunge anazuru maeneobunge mengine wikendi au wakati wa hafla rasmi ya bunge.
Hata hivyo, marupurupu hayo yalisimamishwa Juni mwaka huu baada ya malalamishi kuhusu usimamizi mbaya kutoka kwa walinzi na madereva huku wakiwalaumu mabosi wao, wabunge.
“Kutokana na nilichobaini, sehemu kubwa ya wabunge hawataki kugusa hela hizo na ninawashauri kwa sababu tu itawasababishia matatizo hatimaye,” Spika Wetang’ula aliwaonya wabunge waliomsikiza kwa makini.
Suala hilo lilizuka baada ya Mbunge wa Thika Town, Alice Ng’ang’a, anayehudumu muhula wake wa pili, kumtaka Spika kufafanua ni nani atagharamia matumizi ya madereva na walinzi walioandamana na wabunge Naivasha.
IMETAFSIRIWA NA MARY WANGARI