Habari za Kitaifa

Yaya atoweka na mtoto wa umri wa mwaka mmoja Nyeri

June 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MERCY MWENDE

KWA wiki moja sasa, Bi Joyce Wanjeri amekuwa akimtafuta mwanawe wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba kote mjini Nyeri bila mafanikio.

Inadaiwa kwamba mwanawe, Ian Kariuki, aliibiwa na yaya wa umri wa miaka 46 mnamo Mei 31, 2024.

Juhudi za mama huyo pamoja na zile za Wakfu wa Missing Child Kenya, zimepiga hatua kiasi, wakipata miongozo kuhusu anakoweza kuwa mshukiwa Jane Nyambura, ingawa mafanikio bado.

Polisi pia wanachunguza tukio hilo. Kesi iliripotiwa katika kituo cha polisi wa doria kilichoko Kiamwathi na kunakiliwa kama tukio (OB) nambari 02/01/06/2024.

“Mshukiwa alionekana mara ya mwisho Jumanne, Juni 4, 2024, saa mbili asubuhi katika mji wa Mweiga, Kaunti ya Nyeri, huku akiandamana na mwanamke mwingine aliyekuwa amembeba mwanangu mgongoni. Watatu hao waliingia hotelini na kuitisha chakula,” alisema Bi Wanjeri kwenye mahojiano.

Bi Joyce Wanjeri, mamake mtoto Ian Kariuki aliyepotea. PICHA | JOSEPH KANYI

Hata hivyo, inaaminika kwamba wakiwa katika hoteli hiyo mteja mmoja aliwanunulia chakula na pia akajitolea kumnunulia mtoto huyo unga katika duka la karibu.

Ni baada ya watatu hao kuondoka ndipo mwenye hoteli aligundua kuwa mmoja wa wanawake aliowahudumia ni yule yule ambaye picha yake ilikuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa siku kadhaa.

“Mmiliki wa hoteli hiyo alituarifu na kuthibitisha kwa polisi kwamba mtu ambaye alikuwa amemwona ni huyo huyo mshukiwa ambaye tunamtafuta tangu muda huo wote,” akaeleza Bi Wanjeri.

Taarifa hizo zilitoa mwanga wa matumaini kwa familia hiyo ambayo imekuwa ikitafuta mtoto katika miji ya kaunti hiyo kila inapopokea vidokezo kuhusu aliko mshukiwa.

Bi Wanjeri, ambaye ni mwalimu katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Mathenge huko mjini Nyeri, anasema kuwa katika muda wa miezi miwili iliyopita alimuajiri mshukiwa kama yaya wake na hakuwahi kuwa na wasiwasi wowote.

Picha ya mshukiwa Jane Nyambura, yaya anayedaiwa kutoweka na mtoto Ian Kariuki. PICHA | JOSEPH KANYI

“Bi Nyambura alikuwa mnyamavu, mtu mpenda Amani na hakuwahi kuwasumbua wavulana wangu wawili. Mpwa wake anayeishi mtaani kwetu Kiamwathi ndiye alimpendekeza kwangu nimpe kazi,” akaeleza.

Awali, mshukiwa alifanya kazi kama mtunzaji wa nyanya mmoja anayeishi mjini Chaka katika Kaunti ya Nyeri. Aliacha kazi hiyo baada ya kulalamika kwamba alikuwa akifanyishwa kazi kupita kiasi kwa kupewa kazi za shambani.

Siku ya tukio la mtoto kupotea mnamo Mei 31, 2024, Bi Wanjeri anasema kwamba aliondoka nyumbani kwenda kazini mwendo wa saa mbili kasorobo asubuhi, baada ya kumtayarisha mwanake wa umri wa miaka sita kuenda shuleni.

Alimuacha mtoto mdogo akiwa amelala kwenye kitanda chake. Jukumu la yaya lilikuwa kumwandalia kifungua kinywa, kumlisha, na kisha kuendelea na kazi zake za nyumbani.

“Kwa kawaida yaya anapofanya kazi zake, mwanangu hutumia muda wake mwingi kucheza hapa nyumbani,” akaeleza mzazi huyo.

Shughuli ziliendelea kama kawaida pale nyumbani na Bi Wanjeri anasema habari zilizokusanywa kutoka kwa majirani ni kwamba mtoto alionekana nyumbani saa tano asubuhi.

Lakini mtoto mkubwa aliporudi nyumbani kutoka shuleni saa kumi na moja jioni, hakumpata yaya na nduguye mdogo.

Msako wa kuwatafuta wawili hao ulianza saa tatu usiku Bi Wanjeri aliporejea nyumbani kutoka kazini.

Kilichoshangaza, anasema, ni kwamba mshukiwa aliacha vitu vyake vyote ikiwa ni pamoja na simu yake na hivyo kuwa vigumu kumtafuta.

Hata chakula cha mchana ambacho yaya alikuwa amemuandalia mtoto kilikuwa kimehifadhiwa vizuri kwenye friji.

Kulingana na Bi Wanjeri, yaya wake hakuibua malalamishi yoyote kuhusu kazi yake, isipokuwa mara moja siku sita kabla ya kisa hicho kutokea.

“Nilikuwa tu nimerejea nyumbani kutoka kazini aliponijia akilalamika kwamba mtoto wake alikuwa amefukuzwa shuleni kwa sababu ya karo,” akakumbuka.

Kisha Bi Wanjeri alimpa Sh7,000 ambapo angetoa Sh4,000 kulipia masalio ya karo.

Familia inakiri yaya alijua kumtunza mtoto huyo, kiasi cha kujengeka mshikamano mzuri.

“Mara nyingi mwanangu alikataa kubebwa na mtu yeyote isipokuwa yaya huyo,” akasema mume wa Bi Wanjeri, ambaye ni Bw Michael Kariuki.

Bw Kariuki anasema kwa sasa anawasiliana na familia ya yaya huyo katika mji wa Karatina ambako anatoka.

[email protected]