• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
Zakat Kenya, Premier kuchangisha Sh30m kununulia familia 5,000 mlo wa Iftar

Zakat Kenya, Premier kuchangisha Sh30m kununulia familia 5,000 mlo wa Iftar

NA CECIL ODONGO

ZAKAT Kenya na Benki ya Premier jana zilitia saini ushirikiano unaolenga kukusanya Sh30 milioni kusaidia familia 5,000 za Waislamu ambazo ni maskini wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Premier Bank Osman Duale na Naibu Mkurugenzi wa Zakat Kenya Abdi Shakur Mohamed jana walitia saini ushirikiano huo katika eneo la Mihrab Kilimani, Nairobi. Pande zote zilitoa wito kwa wahisani na Wakenya wajiunge nao kutoa msaada kwa familia maskini.

Ramadhan, ambayo ni nguzo ya nne ya Uislamu, inatarajiwa kuanza Machi 10 na kukamilika April 9 kulingana na mwaandamo wa mwezi. Ramadhan ni mwezi wa tisa kwenye kalanda ya Waislamu na ni wakati ambapo Waislamu hufunga kuanzia kuchomoza kwa jua hadi kutua kwake

Ili kufikisha malengo hayo, Zakat Kenya na Benki ya Premier zinapanga matembezi mwishoni mwa Februari. Matembezi hayo yataanza kutoka msikiti wa Adam hadi uwanja wa Sir Ali Muslim unaopatikana Eastleigh huku washiriki wakitakiwa kununua shati-tao kwa Sh1,000.

“Tunalenga kuzifikia familia 5,000 ambazo zina mahitaji mbalimbali na kuhakikisha kuwa zimepata chakula wakati wa Ramadhan. Huu ni mradi unaohusu jamii na ni kati ya masuala ambayo yanapigiwa upato na benki yetu,” akasema Bw Duale.

“Tunataka kupunguza matatizo ambayo ndugu zetu Waislamu hupitia wakati wa Ramadhan. Lengo kuu ni kuinua na kuboresha maisha yao wakati wa Ramadhan,” akaongeza.

Bw Mohamed naye alisema kuwa wamekuwa wakiendeleza wema huo kwa miaka saba sasa. Alisema ushirikiano na Benki ya Premier utahakikisha kuwa angalau familia hizo zinapata chakula wakati wa Ramadhan.

“Tunashukuru benki ya Premier kwa uamuzi wao. Huu ndio mwanzo wa safari ya kuhakikisha kuwa kila familia maskini inapata chakula wakati wa Ramadhan. Tunaomba Allah atuongoze,” akasema Bw Mohamed.

Alifichua kuwa Zakat imekuwa ikiendeleza mradi huo wa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii kwa miaka saba na itathmini wale wanaotaka msaada huo kabla ya kuchukua hatua na kuingilia kuwasaidia.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Tafsiri na ukalimani zijumuishwe katika...

KAA yapiga mnada ndege zilizokawia maegeshoni

T L