• Nairobi
  • Last Updated June 16th, 2024 7:50 PM
Ziara ya Amerika: Ruto avunia Kenya minofu

Ziara ya Amerika: Ruto avunia Kenya minofu

NA BENSON MATHEKA

ZIARA ya Rais William Ruto nchini Amerika imevunia Kenya uwekezaji na ufadhili wa mabilioni ya pesa kupitia mipango na miradi mbalimbali.

Mipango hiyo inahusiana na ukuzaji wa demokrasia, haki za binadamu na utawala, ushirikiano katika sekta ya afya, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, biashara na uwekezaji, tekinolojia ya dijitali, amani na usalama.

Serikali ya Amerika ilikubali kutumia Sh5.2 bilioni kusaidia mipango ya kukuza demokrasia na haki za binadamu Kenya ikiwemo kulinda uchaguzi wa demokrasia na michakato ya kisiasa, kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi na kukabiliana na dhuluma za jinsia.

Katika kusaidia mashirika ya kijamii, Amerika iliahidi kutumia zaidi ya Sh440 milioni na Sh 169 milioni kwa mipango ya kuwezesha vijana. Vile vile, Amerika itapatia Kenya Sh78 milioni kusaidia watu walio na ulemavu.

Amerika pia imeahidi kusaidia serikali ya Kenya na Sh65 milioni kufanikisha mipango ya kupiga vita ufisadi ikiwemo kufanya mchakato wa kuandaa bajeti kuwa wenye uwazi zaidi na kuhusisha raia zaidi. Serikali ya Rais Joe Biden, pia aliahidi Sh 65 milioni kuwezesha mashirika ya kijamii kuelimisha umma jinsi ya kupiga vita ufisadi.

“Ili kusaidia serikali ya Kenya kupiga vita ufisadi, serikali inatoa Sh32 milioni kupitia mpango wa Global Accountability Program, na Sh 40 milioni kusaidia mpango wa Kenya wa kuwalinda wanaofichua ufisadi. Pia, USAID imetoa mamilioni kusaidia utekelezaji wa sera na sheria zinazohusu ulaghai, uharibifu na matumizi mabaya ya pesa katika utoaji wa huduma za umma kwa raia wa Kenya,” taarifa kutoka Ikulu ya White House ilisema.

Katika ziara iliyokuwa ya kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na Amerika, serikali ya Joe Biden ilitangaza mpango wa Sh280 milioni kwa mpango wa kuleta mageuzi katika idara ya magereza.

Ili kuimarisha amani na usalama, Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki yatakayonufaika na ufadhili wa Sh924 milioni. Ufadhili huo utasaidia mageuzi na kujenga uwezo wa idara ya polisi na sekta ya haki.

Amerika pia imeahidi kusaidia wanaharakati na wanahabari kutayarisha makala ya upekuzi kwa lengo la kufanya Nairobi kuwa kituo cha kufichua masuala muhimu kwa umma. Utawala wa Biden, pia umeahidi kufadhili Kenya kuimarisha mfumo wa uchaguzi huru na wa haki.

“Kwa kushirikiana na Congress (Bunge la Amerika), serikali inanuia kutoa usaidizi wa kiufundi wa Sh198 milioni kwa mchakato wa mfumo wa mageuzi ya kisheria uchaguzini unaolenga kutia nguvu tume ya uchaguzi, vyama vya kisiasa na ufadhili wa kampeni,” ilisema taarifa ya White House.

Amerika, kupitia USAID, imepatia kampuni ya Rivital Healthcare Sh300 milioni kujenga maabara ya kupima Ukimwi, Malaria, Homa ya Dengue, na maradhi ya ini.

Taarifa ya White House ilisema kwamba, serikali ya Amerika inalenga kutumia Sh450 milioni kufadhili wanafunzi 60 wa Kenya kusomea Amerika. Serikali hiyo pia ilitangaza ufadhili wa mabilioni kusaidia sekta ya elimu Kenya hasa sayansi, utafiti na uhandisi.

USAID, kupitia mpango wa Power Africa Initiative, imetoa Sh40 milioni kusaidia wajasiriamaji wanawake na usawa wa jinsia katika sekta ya kawi na ikaahidi Sh470 milioni kuunganisha makazi na taasisi Kenya na stima.

Ili kupunguza gharama ya intaneti, Amerika ilitangaza uwekezaji wa Sh160 milioni Wilken Group kutafuta uwekaji wa nyaya za inteneti yenye kasi.

Amerika pia ilitangaza kuwa Kenya itapokea helikopta 16 zilizotengenezewa Amerika zitakazowasilishwa kati ya 2024 na 2025 kuimarisha uwezo wa kudumisha usalama katika ukanda huu na kushiriki katika kudumisha amani.

Rais William Ruto pia alipata ufadhili wa Sh477 bilioni kujenga barabara kuu ya Nairobi hadi Mombasa kuwa ya laini nne kila upande.
Kenya pia inaendelea kununua vifaa vya kijeshi kutoka Amerika.

Kampuni kubwa za tekinolojia pia zinatarajiwa kuwekeza Kenya na kuunda nafasi za kazi.

Serikali ya Kenya pia itafaidika na ufadhili wa kulinda wanyamapori na kuimarisha mnazingira kutoka kwa serikali ya Amerika.

  • Tags

You can share this post!

Msaada wa Rais wa Sh10,000 uko wapi? ODM sasa wauliza

Majonzi mwili wa mfanyabiashara ukipatikana gesti

T L