HabariSiasa

Hakuna njama ya kumtimua Matiang'i kazini – Duale

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Aden Duale amepinga madai kuwa wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto wanapanga kuwasilisha hoja ya kumfuta kazi Waziri wa Usalama Fred Matiang’i.

Akihutubia wanahabari Jumatano afisini mwake katika majengo ya Bunge, Bw Duale alisema hana habari zozote kuhusu njama ya wabunge wa Jubilee kuwasilisha hoja kama hiyo.

“Kama kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa ningependa kusema wazi kwamba hakuna mpango au mchakato ulioanzishwa kumwondoa afisini waziri yeyote wa Serikali, akiwemo Matiang’i,” akasema.

Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa mjini alisema wanaotoa madai kama hayo ni watu wanaotaka kuingiza siasa katika vita vya ufisadi vinavyoendelea na uchunguzi kuhusu sakata ya dhahabu feki.

“Nawaomba watu kukoma kueneza uvumi ambao hauna msingi. Hizi ni njama za kunyumbisha vita dhidi ya ufisadi na kuingiza siasa katika uchunguzi kuhusu sakata ambapo watu wengine inadai walilaghai famili ya kifalme Dubai,” akasema.

Mnamo Jumatatu kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi alisema kuna njama inayosukumwa na Naibu Rais William Ruto kumwondoa Waziri Matiang’I afisini.

“Wafuasi wa Naibu Rais wanataka kutumia uwepo maafisa wa elimu katika nyumba ambako dhahabu feki ilipatikana mtaani Kileleshwa kama msingi ya kudai wanataka kumwondoa Matiang’I kwa kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini (ODM).

“Ikiwa wanataka kumwondoa Matiang’I sharti wawe na sababu thabiti. Lakini wajue kwamba hatutawaruhusu kufanikisha njama hiyo. Wabunge wa upinzani wataungana na wale wa Jubilee wanaomuunga Rais Uhuru Kenyatta kuangusha hoja kama hiyo,” akawaambia wanahabari afisini mwake.

Bw Mbadi alisema Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Belgut Nelson Koech ndio wanaongoza mchakato wa kukusanya sahihi kuwezesha kuwasilishwa kwa hoja hiyo.

Lakini alipofikiwa kuhusu madai hao, Bw Koech aliungama kuwa suala hilo la kumwondoa Matiang’I afisini linajadiliwa.

“Wengine wetu tunaamini kuwa Waziri Matiang’I amevika wajibu wake. Na ninaweza kukumbia kuwa kuna majadiliano ya kina yanayoendelea kuhusu hatima yake,” akasema.

Naye Bw Nyoro alikataa kukana wala kukubali uwepo mwa mpango kama huo.

“Sitasema lolote wakati huu. Naomba msubiri yatakayotokea siku za hivi karibuni,” akasema.