Hali tete wakimbizi 40, 000 kutoka Ethiopia wakifurika Moyale
TUME ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) imetaka hatua za dharura za kibinadamu kuchukuliwa huko Moyale, Kaunti ya Marsabit, huku idadi ya raia wa Ethiopia wanaotoroka mapigano nchini mwao ikikadiriwa kufikia 40,000.
Tume hiyo inasema takriban watu 15,000 wanaishi katika kambi za muda huku zaidi ya 20,000 wakihifadhiwa na marafiki na jamaa.
Naibu Kamishna wa Kaunti ya Moyale, Benedict Munywoki, alisema mapigano yanaendelea huku milio ya risasi na mabomu ikisikika mara kwa mara, na kulazimisha watu zaidi kuvuka mpaka kutafuta usalama.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Kenya amekadiria idadi ya waliotoroka makazi yao imefikia 36,000.
Mwenyekiti wa KNCHR, Claris Ogangah, alisema ongezeko hilo limeweka shinikizo kwa rasilimali zilizopo, hasa chakula, maji safi, makazi, usafi na huduma za afya.
Alionya kuwa mvua inaweza kuzidisha changamoto za usafi na kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa.
Tume hiyo imetaka wakimbizi wahudumiwe kwa heshima na kupewa chakula, maji safi, makazi na matibabu yanayofaa.
Wakati huo huo, Baraza la Wazee la Borana limetaka Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kuchunguza wabunge Farah Maalim na Hussein Weytan kwa madai ya kutoa matamshi yanayoweza kuchochea uhasama kuhusu mzozo wa Ethiopia.
Wazee hao wanaonya kuwa matamshi ya viongozi yanaweza kuongeza taharuki katika maeneo ya mpakani. Usalama umeimarishwa Moyale huku maafisa zaidi wa polisi wakitumwa eneo hilo.