Habari

Hamna afueni ya maana Epra ikipunguza bei ya petroli kwa Sh1 tu

Na CHARLES WASONGA August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imepunguza bei ya petroli na mafuta taa kwa kima cha Sh1 pekee huku bei ya dizeli ikasalia ilivyokuwa kuanzia Julai 15, 2025, hatua ambayo haitoi afueni yoyote kwa raia.

Kwa hivyo, kulingana na bei hiyo mpya iliyotangazwa Alhamisi, Agosti 14, 2025, na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA), petroli, dizeli na mafuta taa zitauzwa kwa bei ya rejareja ya Sh185.31, Sh171.58 na Sh155.58 kwa lita, mtawalia,  jijini Nairobi kuanzia Agosti 15 hadi Septemba 14, 2025.

Kuanzia Julai 15 hadi Agosti 14, 2025, wateja jijini Nairobi wamekuwa wakiuziwa petroli, dizeli na mafuta taa kwa Sh184.31, 171.58 na 155.58, mtawalia.

Hii ni baada ya Epra, mnamo Julai 14, 2025, kuongeza bei ya kwa kiwango cha juu cha Sh8.99 kwa petroli, Sh8.67 kwa dizeli na Sh9.65 kwa lita kwa mafuta taa.

Mamlaka hiyo ilisema kuwa ongezeko hilo la bei ya mafuta lilichangiwa na kuongezeka kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa kutokana na vita kati ya Iran na Israel.

Kulingana na Epra, ilipunguza bei ya petroli Alhamisi kufuatia kushuka kwa bei ya bidhaa hii inayoingizwa kutoka ng’ambo kwa kima cha asilimia 1.06 “kutoka dola 716.03 (Sh93,083.9) kwa lita 1000 mnamo Juni 2025 hadi dola 708.47 (Sh92,101.1) mnamo Julai 2025 kwa lita 1000.”

“Kwa upande mwingine, bei ya dizeli ilipanda kwa kima cha asilimia 1.52 kutoka dola 682.73 (Sh88,754.9) hadi dola 693.82 (Sh90,196.6) kwa lita 1000 huku bei ya mafuta taa ikipanda kwa kima cha asilimia 1.87 kutoka dola 692.80 (Sh90,064) hadi dola 705.74 (Sh91,746.2) kwa lita 1000,” ikaeleza Epra.

Bei ya mafuta huathiri hali ya uchumi pakubwa husasan gharama ya uchukuzi na uzalishaji bidhaa viwandani. Sababu ni kwamba magari na mashine hutumia ama petroli au dizeli.

Aidha, mitambo ya uzalishaji wa kawi ya stima hutumia dizeli.