Habari

Harambee Stars yang'ara zaidi ya Taifa Stars

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na GEOFFREY ANENE

KENYA iliishinda Tanzania kwa jumla ya magoli 3-2.

BAADA ya kukesha hadi usiku wa manane, Wakenya walienda kulala wakiwa wamejawa na tabasamu kufuatia ushindi wa timu yao ya Harambee Stars wa mabao 3-2 dhidi ya Tanzania katika mechi ya kusisimua ya Kombe la Afrika (AFCON) jijini Cairo nchini Misri, Alhamisi usiku.

Mitandao ya kijamii ilikuwa na shughuli nyingi, huku waliokuwa maeneo mbalimbali ya kushabikia yakiwemo nyumbani, ofisini na katika sehemu za burudani wakisikika wakishangalia kwa kupiga kelele na wengine kupuliza vuvuzela na filimbi kila bao lilipofungwa na vijana wa Sebastien Migne na pia kuelezea kero lao Tanzania ilipoona lango.

Taifa Stars ya Tanzania ilitangulia kuacha Wakenya na mshangao pale Saimon Msuva aliwaweka kifua mbele dakika ya sita.

Mashabiki wengi walilaumu beki wa pembeni kulia David ‘Calabar’ Owino na kipa Patrick Matasi kwa bao hili pamoja na bao la pili ambalo nyota Mbwana Samatta alipachika dakika ya 40 Wakenya wakiwa bado wanasherehekea bao lao kwanza lililofungwa kwa ustadi na mshambuliaji Michael Olunga dakika ya 39.

Olunga, ambaye alitajwa mchezaji bora wa mechi hii ya Kundi C, alifungia Kenya bao la ushindi dakika ya 80.

Katika mchuano huu, ambao majirani hawa waliingia wakiwa wanauguza vichapo baada ya Kenya kulimwa na Algeria 2-0 nayo Senegal ikapokeza Tanzania kipigo sawia, Matasi na mwenzake kutoka Tanzania Aishi Manula walikuwa na shughuli nyingi michumani kutoka na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka pande zote.

Msuva, Samatta, Erasto Nyoni, Hassan Ramadhani na Mudathir Abbas walimpa Matasi shughuli nyingi langoni, huku Manula akijaribiwa vilivyo na Erick ‘Marcelo’ Ouma, Olunga, ambaye pia alipiga mlingoti, Ayub Timbe, John Avire na Johanna Omolo.

Kenya ilipata bao la kwanza kutokana na frikiki ya Timbe ambayo Manula alikuwa amepangua kabla ya Olunga kupiga makasi safi ndani ya kisanduku. Winga huyo matata kutoka klabu ya Beijing Renhe pia alichangia katika bao la pili baada ya kuchota kona safi iliyojazwa kimiani na Omolo kupitia kwa kichwa. Olunga alitumia guu lake kali la kushoto kufunga bao la ushindi baada ya kumegewa pasi murwa kutoka kwa Eric Johanna Omondi nje ya kisanduku na kuvuta kiki safi hadi wavuni.

Mashabiki wa Kenya, hata wale walioidharau Harambee Stars kabla ya mechi wakisema itavuta mkia kwenye kundi lake, waliweka kando hisia zao na kuvalia uzalendo wa Kenya.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alikuwa mmoja wa mashabiki waliopongeza Migne na vijana wake kwa ushindi huo. Bwana Odinga alisema, “Ulikuwa mchezo wa kuridhisha sana kutoka kwa Harambee Stars uliochangiwa pakubwa na kutokufa moyo baada ya kuwa chini mara mbili na kupata ushindi tuliostahili. Pongezi! Wakenya wako nyuma yenu. Kila la kheri mnapojitahidi kufuzu kwa raundi ya 16. Hongera.”

Naye Naibu Rais Dkt Ruto alisema, “Napongeza Harambee Stars kwa moyo wangu wote kwa kuchapa Tanzania 3-2 na kuweka Kenya katika nafasi ya kupigania tiketi ya raundi ya 16-bora. Kila la kheri mnapojiandaa kwa mechi ya kuamua hatima yetu dhidi ya Senegal.”

Baada ya mechi, mshambuliaji wa Kashiwa Reysol, Olunga alisema kwamba walipata msukumo kutoka kwa mashabiki na “tunatumai kufika mbali iwezekavyo kwenye mashindano haya.”

Nahodha Wanyama kutoka Tottenham Hotspur alisema, “Tumeonyesha moyo wa kupigania matokeo mazuri na uwezo wetu. Inaonyesha kwamba sisi ni wazuri sana kila mtu akijitolea. Nashukuru sana mashabiki kwa kazi nzuri ya kutupatia moyo wa kupigana hadi dakika ya mwisho. Nawaomba waendelee kutupatia mchango huu.”

Kuhusu mechi ya mwisho ya kati ya Kenya na Senegal itakayosakatwa Julai 1, Wanyama alisema, “Itakuwa fainali kwetu. Tutajituma vilivyo kuhakikisha tunapata kitu kizuri kutoka mechi hiyo. Ushindi dhidi ya Tanzania umeongeza imani yetu.”

Mfaransa Migne amesema, “Mechi kama hizi (dhidi ya Tanzania) ni thibitisho kuwa haustahili kufa moyo. Mechi yetu ijayo dhidi ya Senegal ni ngumu na tunastahili kumakinika zaidi.”

Kenya ilishuka uwanjani 30 June jijini Cairo saa chache baada ya Senegal ya kocha Aliou Cisse kupoteza 1-0 dhidi ya Algeria kupitia bao la Youcef Belaili lililopatikana dakika ya 49.

Baada ya matokeo ya Kundi C ya Alhamisi ni kwamba Algeria imeingia raundi ya 16-bora ikisalia na mechi dhidi ya Tanzania hapo Julai 1. Imezoa alama sita. Iko alama tatu mbele ya Senegal, ambayo inatoshana na Kenya kwa alama, ingawa ina tofauti nzuri ya mabao. Tanzania inavuta mkia na imeaga mashindano.

Mataifa 24 yanashiriki makala haya ya 32. Timu mbili za kwanza kutoka makundi sita zitaingia 16-bora, huku timu zingine nne zitakazokamilisha mechi za makundi katika nafasi ya tatu zikiwa na alama nyingi pia zikipata nafasi ya kuwania tiketi ya kuingia robo-fainali.

Nigeria ilikuwa timu ya kwanza kuingia raundi ya 16-bora ilipolemea Guinea 1-0 Juni 26. Ilikuwa imekanyaga Burundi 1-0 katika mechi ya ufunguzi.

Wenyeji Misri pia walifuzu Juni 26 baada ya kulipua DR Congo 2-0. Mafirauni hawa walianza kampeni kwa kulima Zimbabwe 1-0. Misri iko katika Kundi A, ambalo pia liko na Uganda inayoshikilia nafasi ya pili kwa alama nne baada ya kugawana alama na Zimbabwe katika sare ya 1-1. Waganda walipepeta DR Congo 2-0 katika mechi yao ya kwanza.

Zimbabwe ina alama moja nayo DR Congo haijapata kitu. Nigeria inaongoza Kundi B kwa alama sita ikifuatiwa na washiriki wapya kabisa Madagascar, ambao walikaba Guinea 2-2 Juni 22 na kulaza washiriki wengine wapya kabisa Burundi 1-0 Juni 27. Guinea imevua alama moja nayo Burundi bado inatafuta alama ya kwanza.

Miamba Morocco na Ivory Coast watakutana leo Ijumaa katika mechi ya Kundi D ambayo mshindi ataingia 16-bora. Atlas Lions ya Morocco ililipua Brave Warriors ya Namibia 1-0 nayo Elephants Ivory Coast ikachapa Bafana Bafana ya Afrika Kusini 1-0 katika mechi zao za kwanza. Namibia na Afrika Kusini pia zitapepetana leo.

Kundi E linajumuisha Mali (alama nne), Angola (moja), Tunisia (moja) na Mauritania (sifuri). Tunisia na Mali zitachapana leo, huku washiriki wapya kabisa Mauritania wakikabana koo na Angola hapo Jumamosi.

Kundi la mwisho linaleta pamoja Cameroon, ambao ni mabingwa watetezi, Benin, Ghana na Guinea-Bissau. Indomitable Lions ya Cameroon ya kocha Clarence Seedorf ilicharaza Guinea-Bisau 2-0 nayo Ghana ikakubali sare ya 2-2 dhidi ya Benin katika mechi zao za kwanza.