Hata sisi tunataka bonasi, wakulima wa miwa Pwani waambia serikali
WAKULIMA wa miwa kutoka eneo la Pwani wameilaumu serikali kwa kuwadhulumu na kutengwa katika mpango wa kulipa bonasi ya miwa uliozinduliwa hivi majuzi na Rais William Ruto.
Mpango huo, ambao unalenga kuwasaidia wakulima na kufufua sekta ya kilimo cha miwa, ulielekezwa kwa viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali pekee, huku viwanda binafsi vikiachwa nje.
Wakulima hao, kupitia wawakilishi wao, wamemtaka Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe kujumuisha viwanda binafsi kama vile Kampuni ya Sukari ya Kwale (KISCOL) kwenye mpango wa kulipa bonasi hiyo.
“Kwale hatuna viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali. Tunategemea KISCOL, lakini tumeachwa nje ya mpango huu,” akasema mkulima mmoja kutoka Kinondo, Kaunti ya Kwale.
Mkulima kutoka Lunga Lunga, Chai Mwachiro aliiomba serikali kuangalia upya vigezo vya mpango huo ili kuwafaidi wadau wote wa sekta ya sukari.
Kwa mujibu wa Rais William Ruto, bonasi hiyo itahusishwa na utendaji wa viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali, na kugawanywa kulingana na kiasi cha miwa kinachosambazwa na wakulima.
“Mwaka jana, Kenya ilifikia rekodi ya uzalishaji wa sukari tani 832,000. Mpango wa bonasi utawahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji, na kuchangia sekta hiyo kujitegemea na kusafirisha bidhaa nje ya nchi ifikapo 2026,” alisema.
Bw Mwachiro alieleza kuwa siyo haki kutengwa, ikizingatiwa mchango wa kampuni hiyo na wakulima wake wa miwa katika sekta ya sukari.
“KISCOL imepanua shughuli zake za kusaga miwa hadi miezi 11 mwaka huu, ikiwasaidia wakulima 1,500. Ni haki tuhusishwe kwenye mpango wa kulipwa bonasi. Serikali lazima iweke wazi jinsi mfumo huu unavyokusudiwa kuinua wakulima wote,” alisema Bw Mwachiro.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Miwa Kwale, Bw David Ndirangu alisema kuwa kuna ukuaji mkubwa katika kilimo cha miwa eneo la Pwani. Miaka mitatu walitumia ekari 2,682, mwaka jana ekari 4,686 zikitumika.
Pia, wakulima hao, walieleza shauku yao kuhusu usawa wa kugawa asilimia 50 ya kodi ya kila mwaka ya viwanda kwa wakulima, kama ilivyoainishwa kwenye mfumo huo, ikizingatiwa kuwa unatumika tu kwa viwanda vya umma.