Hatua ya kufungua shule yapingwa kortini
Na GEORGE ODIWUOR
WANAHARAKATI wawili kutoka Kuanti ya Homa Bay wamewasilisha kesi mahakamani, wakitaka mpango wa kufunguliwa kwa shule kuanzia Jumatatu ijayo usimamishwe.
Michael Kojo na Evance Oloo wanadai shule nyingi hazijatimiza masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Homa Bay, Thomas Obutu na kuratibiwa kuwa ya dharura.
Wawili hao wanataka mahakama imwamuru Waziri wa Elimu, George Magoha atangaze tarehe mpya ya kufunguliwa kwa shule na wanapendekeza iwe Januari 2021.
Wazazi na wanafunzi wengi walipokea habari za kurejelewa kwa masomo kuanzia Jumatatu bila kutarajia.
Kulingana na Prof Magoha, watakaofungua Jumatatu ni Kidato cha Nne, Darasa la Nane na Gredi ya Nne.
Wanafunzi wengine watasubiri ushauri wa serikali kuhusu tarehe watakayorudi shuleni.
Bw Kojo na Bw Oloo wameelezea hofu kuhusu usalama wa wanafunzi watakaorejelea shuleni, wakisema mikakati haijawekwa ya kuwakinga dhidi ya maambukizi.
Walisema mapendekezo ya kufungwa kwa shule yalitolewa na Wizara ya Afya na ni wizara hiyo hiyo inayopasa kutoa mapendekezo ya kufunguliwa kwa shule.
“Kufunguliwa kwa shule wakati huu kutaweka wanafunzi katika hatari ya kuambukizwa,” Bw Kojo akaandika katika hati za kesi.