Hatujajiondoa uchaguzi mdogo wa Malava, DCP yasema
CHAMA cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kimepuuzilia mbali ripoti kwamba mwaniaji wake katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Malava Edgar Busiega amejiondoa kwenye kinyang’anyiro.
Kwenye taarifa aliyotoa Jumapili, Septemba 14, 2025, Katibu Mkuu wa chama hicho Hezron Obaga alisema habari hizo ni uvumi tu unaosambazwa kwa lengo la kupotosha umma.
Alieleza kuwa propaganda hizo zinaenezwa na wapinzani wao ambao wamehofia kushindwa “kutokana na kupanda kwa umaarufu wa Bw Busiega.”
“Bw Busiega angali kinyang’anyironi na tuko na imani kwamba atashinda mnamo Novemba 27, 2027. Na tunawaomba wafuasi wetu na watu wa Malava kupuuzilia mbali habari hizo za kupotosha na wasubiri kushiriki uchaguzi,” Bw Obaga akaeleza.
Hayo yanajiri siku chache baada ya Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala kuitaka chama cha Democracy Action Party (DAP-K) kuondoa mgombeaji wake Seth Panyako ili kumpisha Bw Busiega.
Lakini kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa amekuwa akishikilia kuwa DCP ndio inapasa kuondoa mgombeaji wake kwa sababu Bw Panyako ndiye anayo nafasi bora ya kushinda kiti hicho.
“Mwaniaji wetu, Seth Panyako ndio anafaa kupeperusha bendera ya upinzani katika kinyang’anyiro eneo bunge la Malava. Ndiye alikuwa nambari mbili katika uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya kushindwa na marehemu Malulu Injendi kwa kura chache mnamo,” akaeleza.
Mnamo Jumatano, DCP ilijiondoa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Mbeere Kaskazini na kutangaza kuwa itamuunga mkono mwaniaji wa chama cha Democratic Party (DP) Newton Kariuki, almaarufu Karish.
Aidha, chama hicho kilitangaza kuwa kitamuunga mkono mgombeaji wa Wiper katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Wadi ya Mumbuni, Machakos.
Na katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Chwele/Kabuchai, chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kilisema kitamuunga mkono mgombeaji wa DAP-K.