Habari

Hatutawarejesha nchini Wakenya walio Wuhan – Serikali

February 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI haitawarejesha Wakenya 100 ambao wamezuiliwa jijini Wuhan, China kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni Raychelle Omamo Alhamisi aliwaambia wabunge kwamba ubalozi wa Kenya kwa ushirikiano na serikali ya China utaendelea kufuatilia hali yao ya kiafya hadi wakati ambapo “serikali itaamua kuhusu hatima yao.”

Waziri Omamo aliwaambia wabunge hao ambao ni wanachama wa Kamati kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kimataifa kwamba balozi wa Kenya China Bi Sarah Serem amekuwa akijulisha wizara yake kuhusu hali ya Wakenya hao kila mara.

“Kufikia sasa, serikali haijafikia uamuzi kuwarejesha Wakenya hao, wanafunzi 91 na wanasarakasi tisa, nyumbani. Lakini wako salama na hawajaambukizwa virusi vya corona,” akawaambia wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kajiado Kusini Katoo Ole Metito.

Waziri Omamo alisema yeye wenzake katika wamebuni kamati ndogo ya kujadili mbinu za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

“Kamati hiyo ya mawaziri inafanya kazi kwa ushirikiano na Kamati ya Kiufundi ya Wizara ya Afya ambayo inaendelea kutafuta suluhu kwa kero la virusi hivi kwa Wakenya humu nchini na mataifa ya ng’ambo,” akaongeza.

Bi Omamo aliongeza kuwa Serikali ya China imeanzisha laini 41 za mawasiliano ya dharura ambayo wanafunzi hao wanaweza kutumia kusaka usaidizi kutoka kwa maafisa wa serikali ya China.

“Vile vile, wanafunzi hao wameanzisha kundi la mawasiliano kupitia mtandao wa kijamii kwa jina “WeChat” (sawa na WhatsApp) ambako wanaweza kutumia kusaka usaidizi kuhusu ushauri nasaha kutoka kwa serikali ya China,” akaongeza.

Bi Omamo aliongeza kuwa Serikali imetoa Sh1.3 milioni kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi hao walioko jijini Wuhan wagharamie mahitaji yao ya kimsingi kama vile chakula.

“Kila mwanafunzi tayari amepokea ruzuku ya Sh15,000. Serikali ya China na Chuo Kikuu cha Wuhan wanawapa wanafunzi hao ufadhili zaidi na vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi kama vile barakoa,’ akaongeza.

Hata hivyo, wabunge walisema hawajashawishika na maelezo ya Waziri Omamo wakisistiza kuwa serikali inapasa kuwarejesha Wakenya 100 walioko jijini Wuhan.

“Mataifa yote yameondoa raia wao kutoka Wuhan na hivyo serikali inapasa kuwarejesha raia wetu nyumbani. Hatutaki kusikiza maelezo ambayo hayana mashiko yoyote kutoka kwa Waziri Omamo,” akasema Mbunge wa Belgut Nelson Koech.

Kauli ya Mbunge huyu iliungwa mkono na wenzake John Kiarie (Dagoreti Kusini), Charles Kilonzo (Yatta) na Peter Mwathi (Limuru).

Bi Omamo alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kujibu maswali kutoka kwa Mbunge Mwakilishi wa Nandi Dkt Tecla Chebet ambaye, miongoni mwa masuala mengine, alitaka kujua hatua ambazo serikali inachukua kuhakikisha kuwa Wakenya 100 walioko jijini Wuhan ni salama.

Kuhusu abiria 239 ambao waliwasili humu nchini Jumatano kwa ndege ya Shirika la China Southern Airline, Bi Omamo alisema kuwa watu hao walifanyiwa ukaguzi katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kabla ya kukubaliwa nchini.

Bi Omamo aliongeza kuwa hafahamu uraia wa abiria hao ambao waliwasili nchini kwa ndege hiyo.

“Ndege iliyowasilisha nchini jana (Jumatano) ilitimiza masharti yote ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini. Abiria wote waliamuriwa kujitenga kwa siku 14 kwanza kabla ya kutangamana na wananchi. Na kwa sababu baadhi ya abiria walikuwa wamevalia barakoa (facemask) siwezi kubaini ikiwa ni wa asili ya India, China, Elgeyo Marakwet au Kisumu,” akasema.